Tuesday, March 22, 2016

KIPINDUPINDU CHAENDELEA KUUA MKOANI IRINGA


NA RAYMOND MINJA IRINGA 
Idadi ya waliokufa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika tarafa ya Pawaga, wilaya ya Iringa  mkoani Iringa imeongezeka na kufikia watano baada ya mgonjwa wengine kufariki na kuzikwa jana kijiji cha Luganga.

Akizungumza na  Mtanzania  kwa njia ya simu Mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Robert Salim alisema wagonjwa watatu wamefia kwenye vituo vya afya na wawili walifia majumbani na kufanya idadi kufikia watano.
Awali akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema usiku wa kuamkia jana mgojwa mmoja  alifikishwa zahanati ya kijiji cha Luganga lakini baada ya muda mfupi alifariki dunia .
Kutokana na kifo hicho idadi imeongezeka na kufikia watano ambapo awali mgonjwa wa kwanza alifariki kutoka kijiji cha Mboliboli na wa pili alikufa wakati akiwa njiani kuelekea Ruvuma na wa tatu amefia zahanati ya kijiji cha Luganga.
Masenza alisema mgonjwa huyo alifikishwa kwenye zahanati hiyo kwa kuchelewa sana akiwa na hali mbaya ambapo waganga walijitahidi kumsaidia lakini ilishindikana na hatimaye kupoteza maisha .
Alisema kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo kunasababishwea na watu wanaokunywa pombe mafichoni na wengine wanagoma kunywa maji yenye dawa ya water guard wakilalamika kuwa yanatoa harufu  kali
.
Afisa Afya wa wilaya ya Iringa Sospeter Tiara akizungumza kwenye shughuli ya mazishi ya Mario Chaula (55) alisema ni vema wakazi wote wa tarafa hiyo kutumia dawa ya kutibu maji ya water guard ambayo wamegawiwa au kuchemsha maji.
Alisema pia wajitokeze haraka kwenye vituo vya afya pale wanapoona kuna mgonjwa wanayehisi kuwa ana kipindupindu badala ya kukaa naye nyumbani na akizidiwa ndio hukimbilia hospitali.
Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Iringa Pudensiana  Kisaka alisema waliougua ugonjwa wa kipindupindu tangu kulipuka kwa ugonjwa huo ni 527.
Kisaka alisema wanatumia viongozi wa vijiji kwa ajili ya kuhakikisha elimu ya jinsi ya kujikinga na kipindupindu inamfikia kila mwananch mmoja mmoja.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More