Wednesday, March 23, 2016

CCM na CUF Watwangana Ngumi Pemba Wakati Wakisherehekea Ushindi wa Dr. Shein

Jeshi la Polisi jana walitumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya amani baada ya wananchi kuanza kupigana kwa sababu za kisiasa wakati wakisherehekea ushindi wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, katika kijiji cha Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni, Pemba.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid Salim, alidai vurugu hizo zimesababishwa na wanachama wa CCM kutoka katika kijiji cha Kwale wilayani humo.

Alisema baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa marudio, wanachama wa CCM katika kijiji cha Kwale, walianza kukusanyika na ngoma zao na kuanza safari ya kuingia katika kijiji cha Mjini Wingi, sehemu ambayo ni ngome ya wanachama wa CUF, huku wakisherehekea kwa kurusha 'vijembe' (maneno ya kejeli) na matusi.

“Pamoja na kutakiwa kuacha matusi wakati wakisherehekea ushindi wa Dk. Shein, waliendelea na kusababisha wenzao kupandwa na ghadhabu kuwachemka na kuanza kupigana,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, wanachama wa CCM kutoka kijiji cha Kwale, walilazimika kukimbilia Kituo cha Polisi Micheweni.

Alisema askari walipofika eneo la tukio, walianza kupiga mabomu ya kutoa machozi na kuvunja milango ya nyumba.

Mwenyekiti huyo alisema nyumba 15 zilivunjwa milango wakati wakiwasaka watu waliokuwa wakihusishwa na vurugu hizo ambazo zilianza kufanyika saa 10:00 jioni na kuendelea hadi usiku juzi.

Aidha, alisema kwa mujibu wa mabaki ya milipuko, jumla ya mabomu 27 yanadaiwa kupigwa mbali na nyumba kuvunjwa milango na kusababisha watu zaidi ya 28 kuyakimbia makazi yao katika kijiji hicho.

“Watu wanne wamekamatwa akiwamo mtoto mwenye umri wa miaka 13, lakini wananchi wengi wamekimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa cha Kojani na Maziwang'ombe,” alisema Rashid.

Hata hivyo, alisema jambo la kushagaza polisi wameamua kuwakamata watu waliofanyiwa fujo badala ya kuwakamata waliokuwa chanzo cha vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba watu watano wanashikiliwa kwa uchunguzi wa kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo, alikanusha kuvunjwa milango 15 pamoja na kutumika mabomu 27 kurejesha hali ya utulivu baada ya wananchi kuanza kupigana.

Waliokamatwa katika mkasa huo ni Kombo Khalfan Faki, Salim Hassan Khamis, Mjawiri Faki, Khatib Dawa Juma na Assaa Bakar Ali, wakazi wa kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis Othman, alisema hali katika kijiji hicho imerejea kuwa ya kawaida na kuwataka wananchi kuendelea na sherehe za kumpongeza Dk. Shein bila ya kuvunja sheria.

Alisema wananchi waliokimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa cha Kojani na Maziwang'ombe, watakuwa ndiyo waliohusika na vurugu na kwamba raia mwema hana sababu ya kukimbia askari.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More