Thursday, March 23, 2017

ZAIDI YA WATU 100 IRINGA WAPATA MAFUNZO YA UKARIMU NA UTALII

WIZARA ya Maliasili na Utalii ipo katika mchakato wa kutunga kanuni zitakazowazuia wafanyakazi wa hoteli wasio na vyeti vinavyotambulika na serikali kutoa huduma katika sekta ya utalii.

Kanuni hiyo ambayo msingi wake unalenga kuendeleza na kuboresha huduma katika ya sekta hiyo, utahusisha pia kuvibana vyuo vya hoteli na utalii ili vitoe mafunzo yanayokidhi viwango.

“Baada ya kutungwa na kuanza kutumika kwa kanuni hizo, waajiri katika sekta hiyo watalazimika kuwaajiri wafanyakazi wenye sifa ambao wamesajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii, Paskas Mwiru.

 Aliyasema hayo jana kwenye mafunzo ya siku tatu ya ukarimu na utalii yanayoshirikisha watoa huduma zaidi ya 100 wanaofanya biashara inayohudumia watalii mkoani Iringa.

Mafunzo hayo yanayotolewa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), yanafanyika kwa siku tatu mjini Iringa.

Mwiru alisema mafunzo hayo ya muda mfupi yameanza kutolewa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya serikali kubaini baadhi ya vyuo vinavyotoa mafunzo hayo; kuyatoa chini ya viwango.

“Pamoja na changamoto hiyo, baadhi ya waajiri wamekuwa wakiajiri wafanyakazi katika sekta hiyo kwa misingi ya udugu na urafiki bila kuzingatia vigezo vya elimu na ujuzi ili kukwepa gharama,” alisema.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’atakia alisema changamoto hizo zimesababisha huduma duni katika maeneo ya mapokezi, chakula, vinywaji na malazi, na hivyo kuleta malalamiko makubwa sana kwa wageni.

Kwa kupitia mafunzo hayo mafupi Meing’ataki alisema; “ni mtarajio yetu maarifa watakayopata washiriki hawa yatawawezesha kutambua wajibu wao ili wageni wanaopata wapate huduma wanazotarajia.”

“Sekta ya utalii ina changamoto nyingi, lakini eneo hili la huduma ni muhimu kwasababu linaweza kusaidia kumrudisha mgeni tena na tena na kumfanya awe balozi kwa watu wengine,” alisema.

Kwa wawekezaji katika sekta hiyo, haitoshi tu kuwa na hoteli kubwa kama itakuwa haina huduma bora kwa wageni wake.

Akifungua mafunzo hayo jana, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Fikira Kissimba alisema licha ya ukanda wa nyanda za juu kusini kuwa na vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wanaovitembelea ni ndogo na moja ya sababu yake ni uduni wa huduma katika sekta hiyo ya utalii.

Akishukuru wizara na SPANEST kwa kutoa mafunzo hayo, Kissimba alisema yatakuwa chachu katika kukuza na kuendeleza utalii kusini mwa Tanzania kwa kutoa huduma bora kwa watalii.

Aliwataka wahudumu katika sekta hiyo waache tabia ya uvivu, kufanyakazi kwa mazoea na wawe wepesi kujifunza ili kuboresha huduma zao.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More