Tuesday, May 10, 2016

Waziri Nchemba Awapasha Wafugaji na Wakulima

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, amewataka wakulima na wafugaji kuacha kutumia uhai wa mtu kama fidia ya mifugo au mashamba yaliyoharibiwa kwa kuuana katika mapigano ya wenyewe kwa mwenyewe.

Nchemba alisema hayo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa baraza jipya la wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi, mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
 
Alisema vitendo vya mauaji ambavyo vimekuwa vikifanywa na jamii za wafugaji na wakulima kuuana havistahili kuendelea kuwapo katika jamii iliyostaarabika.
 
Mwigulu alisema hakuna mifugo wala mashamba yenye thamani zaidi ya maisha ya binadamu, hivyo jamii hizo mbili zinatakiwa kutafuta namna sahihi ya kutatua migogoro baina yao na siyo kuendeleza mapigano na kupoteza maisha ya binadamu wenzao.
 
“Ni aibu sana mtu kuua kwa ajili ya shamba au mifugo kwakuwa hakuna kitu kinachoweza kulinganishwa na maisha ya mtu, hivyo basi fidia za mifugo au shamba zifanyike kwa vitu na siyo maisha ya mtu.”alisema.
 
Mwigulu alisema kuwepo kwa baraza hilo ni matarajio ya serikali kuwa mapigano yaliyokuwa yakisabababisha vifo vya watu wengi yatakomeshwa kwa njia ya marishiano na siyo mapigano.
 
“Niwapongeze sana kwa kuunda chombo hiki kikubwa na cha kitaifa, ni matarajio yangu kuwa kila eneo kuanzia ngazi ya chini litaunda chombo kama hiki kwa ajili ya kutatua kero zenu bila kutoa damu ya mtu,” alisema.
 
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Adam Ole Mwarabu, alisema lengo la kuunda chombo hicho ni pamoja na kulinda haki za makundi hayo.
 
Alisema kuwapo kwa baraza hilo kutasaidia kuondoa uonevu wa kunyang’anywa mifugo, ardhi, nyavu, mazao na kulipishwa faini kubwa bila ya kufuata sheria kwa wahusika.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More