Wednesday, May 18, 2016

Rais Magufuli Atishia Kuwatumbua JIPU Mawaziri Wawili

Operesheni ya kutumbua majipu ya Rais John Magufuli nusura iwaangukie Mawaziri wawili ambao  pia walikuwa  manaibu  mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Taarifa kutoka katika chanzo cha kuaminiwa zimeeleza kuwa Rais Magufuli alionesha kutoridhishwa na utendaji wa Mawaziri hao na kuwafokea mbele ya mawaziri wenzao  kwa kuwataja majina katika kikao maalum cha mawaziri kilichofanyika hivi karibuni.

"Ni mazingira ambayo mawaziri hawakuyazoea kwamba Rais anawaambia moja kwa moja kwa majina, anafoka akisema anaweza kuwafukuza wakati wowote.....

"Mawaziri wamezoea mara kwa mara wanapofanya kosa au uzembe wanaonywa kwa staili tofauti, ni kama ya kistaarabu hivi. Sasa huyu bwana mkubwa hana mchezo, aliwataja kabisa, tena mbele ya wenzao ambao walibaki vinywa wazi.

“Wewe (anataja jina la Waziri) na mwenzako (anamtaja jina pia) nitawatumbua,” Chanzo cha gazeti la Rais Mwema kinamkariri Rais Magufuli.

Mawaziri hao ambao ni wabunge wa kuchaguliwa majimboni kwa upande wa Tanzania Bara, wanaongoza wizara nyeti ambazo zinasimamia sekta mtambuka, wizara ambazo zinagusa sehemu ya ahadi za mabadiliko alizonadi Magufuli wakati akigombea urais katika kampeni za mwaka jana.

Chanzo hicho kilieleza kuwa Rais Magufuli aliwaonya pia mawaziri wengine ambao alionesha kutoridhishwa na utendaji wao kwakuwa hawaendani na kasi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Magufuli alitaka atoe mfano kwa mawaziri wengine kwamba wao si watu maalum sana. Kama wanavyotumbuliwa watu wengine na wao pia wanaweza kutumbuliwa,” kiliongeza chanzo hicho

Rais Magufuli aliunda Baraza lake la Mawaziri mwishoni mwa mwaka jana na kuwashauri wasifanye sherehe ya kuteuliwa kwakuwa wakifanya vibaya hatawaonea haya atawaondoa mara moja bila kujali majina yao.

Utendaji wa Rais Magufuli umeendelea kusifiwa kila kona hususan katika kuwawajibisha viongozi wa ngazi zote na kuonesha nia ya dhati ya kuwahudumia watanzania huku akipambana na uzembe na ufisadi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More