Friday, May 27, 2016

Juma Nkamia Adai Wapinzani Wanasura Mbaya Kiasi Kwamba Wanataka Kutapika na Wengine Meno Yao Yameoza!

Kanuni inayozuia lugha ya kuudhi bungeni ni kiinimacho kwani mbunge wa upinzani akitoa lugha inayokera, mbunge wa CCM ataomba mwongozo kwa Spika na mara akijibiwa atasimama mbunge wa CCM na kutumia lugha hiyo hiyo iliyoombewa mwongozo.

Jana Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) aliporomosha lugha za kuudhi baada ya kuwaambia wabunge wa upinzani waliokuwa wakishangilia kuwa wanasura mbaya hadi wanatamani kutapika.

Akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka 2016/17, Nkamia alionyesha kukerwa na hotuba ya upinzani kuhusu wizara hiyo kwenye sehemu iliyozungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Nkamia alisema uchaguzi umepita na mshindi alipatikana ambaye ni CCM na aliufananisha uchaguzi na mpira kwamba unapoisha uwanjani mtu hawezi kulalamika nje.

“Uchaguzi umeisha, leo mtu anasimama hapa anasema ‘ooh tuliibiwa kura’ mlikuwa wapi wakati mnaibiwa kura?”alihoji na kuwataka wapinzani watafute sababu kwa nini walishindwa na si vinginevyo.

"Wanajua mchezaji mmoja akiumia katika timu unachukua mwingine kwenye timu ile ile lakini inakuwaje unachukua mchezaji kutoka upinzani? Kwa hiyo niwaombe tu muwe mnatafakari kwanza,” alisema.

Hali hiyo iliibua kelele na minong’ono kutoka kwa wapinzani, jambo ambalo lilimlazimu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwataka wabunge huku akiwataja majina watulie ili mbunge huyo amalizie mchango wake.

Nkamia aliendelea, “We nyosha midomo, fanya nini lakini that is the truth (huo ndiyo ukweli). Utaongea sana na utapiga kelele sana lakini ukweli ndio huo na umekuingia vizuri. 

"Mimi kelele wala hazinisumbui. Mimi nataka niwashauri kama wakati ujao mnataka kuwa chama kizuri anzeni kutafuta wachezaji wenu,” alisema.

“Nyie pigeni kelele lakini ukweli ndio huo, wenye akili wanajua na wapiga kelele wanajua na najua limewaingia vizuri sana.”

Kijembe hiki kiliwalenga Ukawa ambao katika uchaguzi mkuu uliopita walimteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa. Ukawa walimteua Lowasa baada ya kuitema na kuihama CCM ambapo alipambana na John Magufuli (CCM) aliyeshinda.

Nkamia akionekana kumlenga mbunge fulani ambaye hakumtaja jina alisema, “We piga kelele, kwanza meno yako yameoza.”

Kwa kuzingatia kanuni, lugha hiyo ni ya kuudhi lakini Dk Tulia asisitiza Nkamia amalizie kuchangia ambapo alitoa mfano wa mwandishi wa vitabu Bernard Taper aliyewahi kusema kwamba kuna watu wakiamka asubuhi wakijiangalia kwenye kioo wanatamani kutapika.

“Sasa nyie mnaoshangilia humu mna sura mbaya na mnatamani kutapika,” alisema Nkamia

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More