Thursday, May 19, 2016

CHADEMA Yajipanga Kumng'oa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema uzito wa Rais John Magufuli kumwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kutokana na kutajwa kuhusika na Kampuni ya Lugumi inayodaiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, utasababisha waanze harakati za kumng’oa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais John Magufuli hana budi kuchukua hatua haraka kumwajibisha Waziri Kitwanga kama alivyofanya kwa watumishi wengine wa umma katika operesheni ya kutumbua majipu.

Waziri Kitwanga anadaiwa kuwa na hisa kwenye Kampuni ya Infosys Ips Tanzania Limited ambayo ilipewa zabuni ya kutoa huduma za kitaalamu na Kampuni ya Kimarekani ya Biometrica kuhusu uwekaji wa mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi. 
Mkataba wa kuweka mashine hizo uliingiwa kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises ambayo ililipwa Sh34 bilioni kati ya Sh37 bilioni za mkataba, wakati kazi ya kufunga mashine hizo ilifanyika kwenye vituo 14 tu hadi wakati Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipofanya ukaguzi.

Hata hivyo, kampuni hiyo inadai kuwa Kitwanga, ambaye ni mmoja wa waasisi wa Infosys, alijiondoa kwenye uendeshaji tangu mwaka 2010, wakati mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011.

Chadema bado inaona kuwa Rais Magufuli anatakiwa kumwajibisha waziri huyo wa Mambo ya Ndani.

“Kama Rais akishindwa kuchukua hatua katika hili, Serikali itang’oka madarakani. Sisi Chadema tutaiondoa. Haiwezekani wakati Lugumi inachunguzwa mhusika mkuu (Kitwanga) aendelee kuwa waziri, tena wa wizara inayohusika na mkataba wa Lugumi,” alisema Mwalimu.

Mwalimu alisema, Rais anapaswa kujitokeza hadharani na kueleza uhusiano wake na Kitwanga na awaeleze Watanzania kuwa kutokana na uswahiba wao ndiyo sababu ya kutomchukulia hatua.

“Mbona anawatumbua marafiki wa wenzake? Kwa nini marafiki zake anashindwa kuwatumbua? Ukiwa kiongozi mwenye kubagua katika uamuzi ni hatari kwa uchumi wa Taifa, ni sawa na baba anayewabagua watoto wake matokeo yake ni kuzalisha chuki tu.”

Licha ya Mwalimu kutotaka kuweka wazi mpango huo, kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
 Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.

Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 372, kati yao wabunge wa upinzani ni 118.

“Hilo tutalifanya iwapo tu Rais atashindwa kumwajibisha Kitwanga. Ila huyu waziri naye anapaswa ajipime mwenyewe ili kumlinda bosi wake (Waziri Mkuu). Afanye kama Edward (Lowassa-waziri mkuu mstaafu) aliamua kujiuzulu wadhifa wake ili kumlinda Jakaya (Kikwete-Rais wa Awamu ya Nne) kwa kosa ambalo yeye hakulifanya,” alidai Mwalimu.

Mwalimu alidai kwamba Serikali imezuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kuhofia uchafu wa viongozi, likiwamo sakata la Lugumi.

“Ndiyo maana tunasema CCM ni ileile maana wametumbua majipu, sasa imebaki mitoki. Ni kama imewashinda maana ipo sehemu mbaya,” alisema.

Licha ya mkakati huo wa Chadema, Aprili 19 mwaka huu, Kitwanga alisema kuwa hahusiki katika sakata hilo na juzi alijibu hoja ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) lililomtaka ajiuzulu, akisema hawezi kuwajibu watoto ili kuonyesha tofauti yake na wao.

Katika maelezo yake, Mwalimu aliorodhesha utumbuaji ambao Rais Magufuli ameufanya tangu aingie madarakani, ukiwamo wa watendaji waliofanya vurugu tu katika vikao kwa kusisitiza kuwa ni ajabu kuona mpaka sasa hajamchukulia hatua yoyote Kitwanga wakati ukweli uko wazi kuwa anahusika na sakata la Lugumi. 
Baada ya ripoti ya CAG kuibua udhaifu huo kwenye mkataba, Kamati ya Hesabu za Serikali ya Bunge iliunda kamati ndogo kufuatilia tuhuma hizo baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuhusu mkataba huo.

Kampuni ya Infosys ni wakala wa kampuni maarufu duniani ya kutengeneza kompyuta ya Dell, ikijihusisha na usambazaji wa vifaa hivyo, matengeneza na utoaji huduma za kitaalamu.

Kaimu katibu mkuu huyo wa Chadema alisema, chama hicho pia kinajipanga kuanza ziara yake nchi nzima na ajenda kuu itakuwa kuanika mambo yote mabaya yanayofanywa na Serikali.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More