Friday, May 6, 2016

Wabunge wa UKAWA Wamzomea Profesa Tibaijuka huku Wakimwita Mwizi.

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka jana alikuwa mkali bungeni akisema yeye si mwizi na kuwabeza wanaomuita hivyo kuwa wataisoma namba.

Profesa Tibaijuka alifikia hatua hiyo baada ya kuhamaki kutokana na baadhi ya wabunge wa upinzani kupaza sauti na kumuita mwizi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Profesa Tibaijuka alianza kwa kuwataka wabunge wamuunge mkono Rais John Magufuli kwa kuwa amechaguliwa na wananchi.

“Wenzetu ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi (upinzani) wana haki ya kusema wanayoyasema, lakini hata sisi tuna haki ya kuyaweka vizuri ili yaeleweke kwa wananchi,” alisema.

Profesa Tibaijuka alisema upinzani ukifilisika utabaki kukemea kwa sababu ni lazima tu useme kitu, Bunge linageuka kijiwe na bungeni si mahali pa kupeleka hoja za vijiweni.

Kauli hiyo iliwakera wabunge wa upinzani ambao walianza kupaza sauti zao dhidi yake, hali iliyoonekana kumchanganya.

Akirejea hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu kuwa Tanganyika inainyonya Zanzibar na kuifanya koloni lake, Profesa Tibaijuka alihoji: “Tanganyika inainyonya Zanzibar katika lipi? Hili ni jambo la kujiuliza. Nimejiuliza mimi kama mchumi. Kazi yangu ya kwanza nyinyi mnanijua nilikuwa kwenye shirika la makazi duniani, hamjui kwamba nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia?” alihoji.

Kutokana na zomeazomea kuendelea, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliingilia kati: “Waheshimiwa wabunge namlinda mzungumzaji, naomba muwe wavumilivu. Mheshimiwa Profesa endelea."

“Kwa wale wanaosema nimeiba mtaisoma namba, mimi si mtu wa kutishwa na vitu vya ovyoovyo.

"Mimi sitishwi na hoja za ovyoovyo, huyo (mtu) akaisome namba. Nasimama hapa kwa sababu nataka nitetee vitu. Mtu anapopotosha anaweza kuleta hatari. Tanganyika kwa mtizamo wa kiuchumi haiwezi kuinyonya Zanzibar.

“Katika Dunia ya ustaarabu unasikia hoja. Lissu hapa angeweza kuzomewa, lakini wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa,” alisema huku baadhi ya wabunge wakiendelea kumzomea.

Tibaijuka aliwahi kuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na aliondolewa baada ya kutuhumiwa kupata mgawo wa fedha za Tegeta Escrow.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More