Tuesday, May 10, 2016

Rais Magufuli Awagomea Wabunge Nyongeza Ya Mikopo Ya Magari

Katika kile kinachoonekana amedhamiria kuendelea kubana matumizi ya serikali, Rais John Magufuli amekataa ombi la kuongeza fedha za ununuzi wa magari kwa wabunge pamoja na fedha za mfuko wa bunge.

Baada ya kuchaguliwa, wabunge walipatiwa milioni 90  za mkopo kwa ajili ya ununuzi wa magari, lakini baadhi yao walieleza kutoridhishwa na kiasi hicho, wakidai hakitoshelezi na kutaka kiongezwe hadi sh. milioni 120.

Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa wabunge waliwasilisha ombi kwa Rais Magufuli kuongezwa fedha lakini ombi hilo limekataliwa.

Chanzo cha kuamini kimedokeza kuwa mmoja wa wabunge wa CCM alimkumbushia Rais Magufuli ombi hilo wakati wa kikao cha chakula cha jioni, kilichofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma.

Chanzo hicho kilieleza kuwa Rais Magufuli alikataa kuwaongezea wabunge fungu hilo kwa madai kuwa serikali yake haina fedha.

Kilieleza pia kuwa Rais Magufuli alikataa kuongeza fungu la mfuko wa jimbo kwa kuwa serikali haina fedha huku akiwataka wabunge kufanya kazi kwa bidii.

"Rais alisema kwa sasa hali si nzuri, amekumbana na changamoto mbalimbali na kutuahidi kulichukua ombi letu, endapo hali itatengemaa atatuangalia kwa sababu hata yeye analitambua hilo kwa sababu alikuwa mbunge."Kilisema chanzo hicho

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More