Thursday, May 5, 2016

Hukumu ya Kesi Kafulila Kupinga Matokeo ya Uchaguzi Itatolewa Mei 17

Mahakama  Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora inayosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, David Kafulila inatarajia kutoa hukumu Mei 17, mwaka huu.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora anayesikiliza kesi hiyo mjini Kigoma, Ferdinand Wambali alisema baada ya pande zote kuwasilisha ushahidi na maelezo yao mahakamani hapo amepanga kutoa hukumu tarehe hiyo.

Kutolewa kwa tarehe hiyo ya hukumu kunatokana na kufungwa kwa utoaji ushahidi wa maelezo ya kesi hiyo ambayo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Ruben Mfune ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, aliwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo.

Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote, Jaji Wambali ameomba kupatiwa muda wa kutosha kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo ili atoe hukumu ya haki.

Katika kesi hiyo Namba Mbili ya mwaka 2015, David Kafulila aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo anaitaka mahakama itengue matokeo yaliyompa ushindi mgombea wa CCM, Hasna Mwilima na badala yake mahakama imtangaze yeye (Kafulila) kama mshindi halali wa uchaguzi katika jimbo hilo.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Mwilima, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeiwakilisha Tume ya Taifa ya uchaguzi.



Katika kesi hiyo, Wakili Kenedy Mfungamtama anamsimamia Mwilima wakati David Kafulila akisimamiwa na Wakili Profesa Abdallah Safari na Daniel Rumenyela.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More