JESHI
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema limeanza kuchukua
hatua kali kwa watu waliohusika na upigaji wa picha wa vifaa vya kijeshi
na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambapo hadi sasa tayari watu
wanne wapo chini ya ulinzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na
Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema kumekuwa na tabia ya
kusambaa kwa taarifa, zisizotakiwa kusambazwa na kusababisha usumbufu
kwa taasisi za Serikali na hasa Jeshi.
“Desemba
3, mwaka huu saa 1:15 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, lilitokea tukio lisilo la kawaida lililotendwa na
wafanyakazi wa shirika la kupokea mizigo la Swiss Port wakishirikiana na
wenzao wa Shirika la Ndege la KLM kwa kupiga picha vifaa vya kijeshi na
kusambaza katika mitandao ya kijamii,” alisema Kanali Lubinga.
Alisema
mizigo hiyo ni mali ya JWTZ na kuagizwa kwake, hakujaanza hivi karibuni
kama baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wanavyoeleza, bali ni
matokeo ya hatua zilizochukiliwa na JWTZ kupitia Wizara ya Ulinzi miaka
sita iliyopita katika mpango wake wa kujenga uwezo wa JWTZ.
“Tunasikitika
kwa tukio hili la watu kujichukulia maamuzi ya kupiga picha kitu
ambacho hakikuwahusu na pia kusambaza picha hizo kwenye mitandao ya
kijamii na kupelekea kujitokeza kwa maoni ya kupotosha jamii,” aliongeza Mkurugenzi huyo katika JWTZ.
Alisema
tabia za kupotosha jamii, zimetokea mara kwa mara na hivyo kuvunja
mshikamano uliopo kati ya Serikali na wananchi wake, jambo ambalo jeshi
hilo halitalifumbia macho.
Alisema
ni kwa msingi huo, wameanza kuwasaka wahusika wote, ambapo tayari watu
wanne wapo chini ya ulinzi na watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho
kwa wengine, kutokana na upigaji wa picha hizo na usambazaji wake.
0 comments:
Post a Comment