MKUU
wa Mkoa wa Katavi, Dk Ibrahim Msengi amewasimamisha kazi maofisa
waandamizi 11 wa Manispaa ya Mpanda akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wake,
Suleiman Lukanga kwa ukiukwaji wa sheria za manunuzi kwa kufanya
ubadhirifu fedha zaidi ya Sh milioni 92.8.
Dk
Msengi alieleza kuwa Lukanga na maofisa 11 wa Manispaa ya Mpanda
wanatuhumiwa kununua gari la kubeba taka ambapo kiasi cha Sh milioni
92.8 zilitolewa kwa manunuzi hewa kwa kampuni hewa.
Wengine
waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Vincent
Kayombo ambaye pia ni Ofisa Elimu (Msingi) wa Manispaa ya Mpanda, Ofisa
Manunuzi aliyetajwa kwa jina moja la Kakulima, Ofisa Mipango, Ferdinard
Filimbi, Mweka Hazina, Bosco Kapinga, Mhasibu Kibi Hamis Msaka na
wajumbe wanne wa Bodi ya Zabuni.
Dk
Msengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa
huo, ameamuru wakati uchunguzi kuhusu tuhuma hizo ukiendelea, watuhumiwa
wote 12 wasitoke nje ya Mji wa Mpanda na wahakikishe wanalipa kiasi
hicho cha fedha kwa kuwa ni fedha za umma.
“Maofisa
hawa wa Manispaa na Mkurugenzi wao wanatuhumiwa kufanya malipo hewa,
ikiwa ni nusu ya fedha zilizotengwa kununua gari hilo hakika wamefanya
kwa makusudi …..
“Sasa
naomba watupishe ili tufanye uchunguzi kwa kuhusisha vyombo mbalimbali
vya dola na wote wawe nje ya ofisi kuanzia sasa, lakini wasitoke nje ya
Mji wa Mpanda…..naagiza pia walipe kiasi hicho cha fedha,” aliamuru.
Uamuzi
huo umechukuliwa na mkuu huyo wa mkoa kutokana na uchunguzi uliofanywa
na tume tatu tofauti zilizoundwa kuchunguza upotevu wa kiasi hicho cha
fedha ambazo ni kati ya Sh milioni 200 zilizotolewa na Tamisemi kwa
ajili ya kununulia gari la taka katika Manispaa ya Mpanda.
Aidha,
Dk Msengi ametoa onyo kwa mtumishi yeyote aliyezoea kufanya ubadhirifu
wa mali ya umma akisema wakae wakijua kuwa siku zao zimetimia na kwamba
tabia hiyo ovu haiwezi kufumbiwa macho.
Katika
uchunguzi wa upotevu huo wa kiasi hicho cha fedha uliofanywa na kamati
tatu tofauti zilizoundwa na RC huyo zilibaini kuwa Kampuni ya Bluecyon
iliyoko Mbezi, Dar es Salaam ilizawadiwa zabuni ya kununua gari hilo.
Uchunguzi
wa Kamati hizo tatu zilizoongozwa na Katibu Tawala Mkoa, Polisi Mkoa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa Bluecyon
ilikuwa haijihusishi na biashara ya magari, bali ni kampuni ya
uchapishaji.
Akizungumza mjini Mpanda, Lukanga alisema, “Nilikuwa
kikazi kijijini baada ya kufika hapa mjini ndipo nimesikia agizo hilo
la Mkuu wa Mkoa kwamba amewasimamisha kazi watumishi 12 wa Manispaa ya
Mpanda nikiwemo na mimi niseme wazi kuwa agizo hilo tumelisikia.
“Hata
kabla ya RC hajatoa taarifa hiyo jana tayari nilikuwa nimeanza
kulishughulikia tangu mwaka jana na tayari baadhi ya watumishi wa
Manispaa wamefikishwa mahakamani. Mgogoro unakuja baada ya mzabuni huyo
kushindwa kuleta gari hilo la kubebea taka….basi nilichukua hatua
ikiwemo kuvunja mkataba na mzabuni huyo na kuhakikisha fedha hizo
zinarudi."
0 comments:
Post a Comment