Tuesday, December 1, 2015

Rais Magufuli Atangaza Kupunguza Wafanyakazi Katika Mshirika Ya Umma Ambayo ni Mzigo kwa Serikali........Posho za Vikao Kamati za Wabunge Zafutwa

SERIKALI ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imeshusha rungu jipya kwa kutangaza uamuzi mchungu wa kupunguza wafanyakazi katika taasisi na mashirika ya umma ambayo yameonekana kuwa mzigo katika utendaji.

Mashirika hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa  Hazina,  Laurence Mafuru,  katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kukumbushana wajibu na kuhakikisha watendaji hawafanyi kazi kwa mazoea na badala yake kutakiwa waendane na mabadiliko ya kiuchumi.

Mfuru aliyataja baadhi ya mashirika hayo mzigo yanayotakiwa kupunguza watumishi wake kuwa ni Shirika la Reli Tanzania (TRL), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Mafuru alisema hayo ni maelekezo ya Rais Magufuli kwa watumishi hao juu ya utendaji anaoutaka katika Serikali ya awamu ya tano.

“Serikali inatarajia kupunguza wafanyakazi kwani kiwango cha utendaji kimeshuka na tusipofanya hivyo jamii inatuona wa ajabu. Kwa mfano kwa sasa Shirika la Reli (TRL), Tanesco, TTCL, NHC, TPA, TPDC wote hawa wanapanga foleni hazina kutaka mishahara maana wameshindwa kujiendesha,” alisema Mafuru.

Alisema Serikali inalipa madeni ya taasisi ambazo zimeshindwa kujiendesha yakiwamo ya pensheni za wastaafu, huku lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kwamba yanaiingizia Serikali mapato na kukuza uchumi wa nchi.

“Taasisi zote zinazopokea mtaji kwa Serikali zinatakiwa kujieleza kwanini zinashindwa kupata faida kwa kuingiza mambo ambayo hayana msingi,” alisema Mafuru na kutolea mfano vyuo binafsi vinavyojiendesha kwa kutegemea michango ya shule na machapisho, huku vyuo vya  Serikali vikitegemea fedha kutoka hazina.

“Ningewasifu sana kama wangeomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo, lakini fedha zinazoombwa ni karatasi na machapisho wakati hivi wangenunua wenyewe kwa lengo la kukuza uchumi wetu,” alisema.

Akizungumzia kuhusu nafasi za uteuzi wa rais, alisema watumishi wengine wanapoteuliwa huchukulia kama wamepewa zawadi wakati wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo.

“Nafasi za uteuzi wa rais si zawadi bali ni kazi, hivyo mtu anatakiwa kufanya kazi kwa weledi, na kama anaona hatoweza kazi hiyo, ni bora aikatae ili apewe mwingine anayeweza kufanya kazi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu majukumu ya mawaziri, alisema ni lazima watambue mipaka katika sehemu zao za kazi ili kuepuka kuingiliana masuala ya utawala kwani kinachoangusha mashirika ya umma ni watu kutofuata utawala bora.

Alisema taasisi za Serikali zinatakiwa kufanya kazi kwa pamoja kwa kuhakikisha zinavunja kuta za kisheria na kiutendaji na kushughulikia kero za wananchi ikiwamo maji, elimu, afya na umeme.

“Ni vyema taasisi zipunguze matumizi hata ya wanasheria kwani zipo taasisi wanasema mwanasheria wao analipwa shilingi milioni tano hadi 20, sasa ina maana mwingine ana kesi nyingi zaidi au inakuwaje?”alisema na kuhoji Mafuru.

Alisema miradi yote yenye uwezo wa kujiendesha haitakiwi kujazana hazina badala yake watumie vyanzo vya mapato walivyo navyo.

Mafuru alisema Serikali itachukua hatua za kuhakikisha kwamba inafufua mashirika hayo ambayo ni mizigo ili kuweza kujiinua na kufikia kiwango stahiki kwani yakisimama vizuri yatasaidia katika kukuza uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.

“Serikali tunapitia madeni yetu tunayodaiwa na mashirika ya umma na tutayalipa, na lazima muhakikishe matumizi yanabanwa kwenye uendeshaji wa mashirika na kufanya manunuzi yenye tija,” alisema.

Aidha aliyataka mashirika ya umma yahakikishe yanakamilisha madeni wanayodaiana wao kwa wao ili kusaidia mashirika ambayo yanadai fedha nyingi kuweza kupata fedha za kuwekeza.

Akitolea mfano wa Tanesco, Mafuru alisema fedha ambazo shirika hilo linadai  katika mashirika na taasisi nyingine zina uwezo wa kutekeleza mradi kama wa Kinyerezi I.

“Unaweza kuona kama madeni yote ya Tanesco yangelipwa, ingekuwa imekamilisha mradi wa Kinyerezi II,” alisema.

Vikao vinne tu vya Bodi
Akizungumzia kuhusu posho za vikao vya bodi, alisema kwa sasa hivi kutakuwa na vikao vinne tu kwa mwaka tofauti na ilivyozoeleka ambapo ikifika Januari kunakuwa na utitiri wa vikao.

Katika kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kutosha, aliyataka mashirika ya umma kupendelea kutumia benki za Serikali kuliko benki binafsi.

Posho za wabunge Zafutwa
Kuhusu wabunge kulipwa posho kutoka hazina pindi wanapokuwa katika vikao vya bodi mbalimbali, alisema kuwa zimepigwa marufuku kwani posho zao wanalipwa na Bunge.

“Mtu mwingine anakuwa kwenye bodi zaidi ya moja kwa sababu anajua kuwa kuna posho, hii haikubaliki, watakuwa wanalipwa posho za Bunge tu,” alisema Mafuru.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More