ULE mpango wa kuuza gari la kisasa
lililokuwa likitumiwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi ili
fedha zitakazopatikana zitumike kununua gari la kubeba wagonjwa kwa ajili ya
hospitali ya manispaa hiyo, umeyeyuka.
Gari hilo aina ya Toyota Landa Cruiser
Prado New Model linaelezwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni 150.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Iringa kiliwalaumu
waliokuwa madiwani wa halmashauri ya manispaa hiyo wa 2010-2015 ambao kwa
asilimia 99 walichaguliwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kupitisha
uamuzi waliouita wa kipuuzi wa kununua gari hilo huku hospitali hiyo ikiwa
haina gari la kubeba wagonjwa.
Katika mikutano yao mbalimbali ya kampeni
Chadema waliwaomba wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini wamchague mgombea wao ubunge
na wagombea wake ili wakafanye maamuzi mengi yenye maslai mapana kwa wapiga
kura ikiwa ni pamoja na kuuza gari hilo kwa lengo la kutumia fedha zake kununua
gari la kubeba wagonjwa.
Ahadi hiyo na nyingine nyingi za chama
hicho zilipokelewa na wapiga kura wa mjini Iringa kwa kumchagua kwa awamu
nyingine ya miaka mitano Mchungaji Peter Msigwa kuwa mbunge wa Jimbo la Iringa
Mjini na kuwachagua madiwani 14 kati ya 18 wa jimbo hilo, kuunda halmashauri ya
manispaa hiyo.
Wakizungumza na wanahabari mwishoni mwa
wiki iliyopita, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe na Naibu wake Joseph Lyata
walisema mpango wa kuuza gari hilo haupo tena kwasababu taratibu za kupata gari
la wagonjwa zinaendelea kufanywa kwa kasi kubwa.
“Ni kweli kulikuwa na ahadi ya kuuza gari
hili ili fedha zake zitumike kununua gari la wagonjwa, mpango huo haupo tena
kwasababu kuna mipango mingine ya kupata fedha zitakazotumika kununua gari
rasmi la wagonjwa,” alisema naibu Meya, Lyata.
Lyata alisema kwa kuzingatia mpango huo, gari
hilo litaendelea kutumika kwa matumizi ya meya, naibu wake na kwa shughuli
zingine za halmashauri pale inapolazimu.
Alisema halmashauri yao itahakikisha
inavipitia vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo, zikiwemo kodi mbalimbali, na
makusanyo yake yatatumiwa kununua gari la kubeba wagonjwa sambamba na kuongeza
gari lingine la kubeba taka ili kuufanya mji wa Iringa uendelee na sifa yake ya
usafi.
0 comments:
Post a Comment