Monday, December 7, 2015

Lowassa Kupigania Ushindi Wa Godbless Lema


Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anatarajiwa kuanza kambi nzito jijini Arusha kuanzia keshokutwa (Jumatano) kwa nia ya kuhakikisha kuwa mgombea ubunge wa chama chake katika katika Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema anatetea kiti chake kwa ushindi wa kishindo.

Taarifa ambazo tulizipata jana toka kwa  watu wa karibu wa Lowassa zilieleza kuwa (Lowassa) ataungana na timu ya kampeni ya Chadema kujichimbia jijini Arusha kwa siku zote zilizobaki za kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo Jumapili ijayo.

Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa Arusha Mjini haukufanyika Oktoba 25, 2015 kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine nchini kufuatia kifo cha mgombea wa ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.  

Kadhalika, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya Lowassa ni muendelezo wa ushiriki wake katika kuiimarisha Chadema kwa nia ya kuleta ukombozi wa kweli kwa Watanzania. 
 
Hivi karibuni alikuwa Mwanza na Geita kwa siku kadhaa katika kushughulikia mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye aliuawa kinyama na watu wasiojulikana.

Katika hatua nyingine, Lema anayegombea kutetea jimbo hilo,alisema ushindi kwake na chama chake uko wazi kwani wananchi wameamka na wengi wamepania kumrejesha madarakani.
 
Alisema kampeni zake za nyumba kwa nyumba ndizo zinazomuongezea uhakika wa kushinda kwani hupokewa vizuri na wote humuahidi kujitokeza kwa wingi Jumapili ili kumchagua.

Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni jana, Lema alisema atakapochaguliwa, kazi kubwa atakayoifanya ni kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri ya Jiji yanaongezeka ili kufanikisha dhamira ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More