Monday, December 7, 2015

Ubunge wa Saed Kubenea Wapingwa Mahakamani

Kubenea

Aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Massaburi, amefungua kesi ya kupinga ushindi wa Saed Kubenea, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Dk. Massaburi amefungua kesi hiyo ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
 
Mbali ya Kubenea, wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni Masimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo, Dk. Massaburi anadai kwamba mshtakiwa wa kwanza (Kubenea), alitoa rushwa ya kununua jenereta katika hospitali ya Mavurunza iliyopo kata ya Kimara, kutoa rushwa ya ujenzi wa barabara ya Matete, kutoa zawadi kwa kununulia  ‘Pool Table’, kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wampigie kura.

Madai dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ni hakumpatia nafasi ya kuhesabu kura upya kama alivyoomba, hakumjulisha tarehe, muda na wapi matokeo ya jimbo hilo yalikuwa yanajumulishwa, yeye na mawakala wake hawakuona wakati vifaa vya uchaguzi vinafunguliwa.

Pia anadai kwamba baadhi ya vituo havikufanya uchaguzi, na pia baadhi ya wapigakura walipiga kura wakati hawajafikisha umri wa kupiga kura.

Katika madai hayo, Dk. Massaburi anaiomba Mahakama Kuu itengue ushindi wa Kubenea uliotangazwa na Msimamzi wa Jimbo hilo.

Akizungumza na mtandao huu jijini Dar es Salaam jana, Kubenea alithibitisha kupokea madai hayo kutoka kwa Dk. Massaburi na kwamba ameombwa kuwasilisha utetezi wake katika mahakama hiyo ndani ya siku 21.

Aidha, Kubenea alisema katika kesi hiyo, atawakilishwa na jopo la mawakili watano akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, Mabere Marando, Peter Kibatala,  Method Kimongoro na Frederick Kihwelo na kwamba wamepanga kuwasilisha utetezi wao ndani ya wiki hii.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More