Waraghbishi
toka kijiji cha Pandagichiza wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya tanki la
maji, ambalo baadhi yao ndio wasimamizi wake kutokana uaminifu wao.
Tanzania
ya leo, imepitia mabadiliko mengi yanayogusa kila sekta tangu ilipojikomboa na
kuwa nchi huru baada miaka 53 ya utawala wa kikoloni. Kwa mfano, katika kipindi
hicho hadi sasa, nchi imeshuhudia kuimarika kwa huduma mbalimbali za kijamii. Kwa
uchache, huduma hizi ni pamoja na afya,
elimu, demokrasia, utalii, viwanda na miundombinu mbalimbali. Katika sekta ya elimu, ongezeko kubwa la shule
kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu limeshuhudiwa. Hii ni moja ya hatua
kubwa kuwahi kufikiwa tangu nchi ilipoanza kujitawala. Katika sekta ya afya,
hospitali, zahanati na vituo vya afya vimejengwa kwa wingi kutegeme mahitaji ya
watu.
Miundombinu
ya barabara imeimarika maradufu na kuifanya Tanzania kuongoza Afrika Mashariki
kuwa na barabara zenye lami kwa kilomita nyingi. Lakini pamoja na mafanikio
hayo, nchi imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali katika kila hatua ya
kujaribu kuboresha huduma na mahitaji ya kijamii. Miongoni mwa changamoto hizo
ni usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ubora wa huduma zinazotolewa.
Viwango vya ubora kwa huduma zinazotolewa, vimekuwa vikipungua kadri siku
zinavyokwenda na sababu kubwa ni udhaifu wa usimamizi kutoka kwa mamlaka
husika.
Udhaifu
huu umesababisha wananchi ambao kimsingi ndiyo walipa kodi za serikali
kulalamika kila siku. Ikumbukwe kuwa ukusanyaji mzuri wa kodi na kuweka
matumizi wazi husaidia kuboresha huduma mbalimbali ndani ya jamii. Ili
kuepukana na utawala mbovu usiojali wala kuheshimu misingi ya utawala bora,
kuna haja ya wananchi kufanya kazi pamoja. Hapa ndipo tunapouona mpango wa
Chukua Hatua kama mkombozi kupita uraghbishi, yaani kuwahuisha na kuwahamasisha
watu walionyimwa haki kujiona kama watendaji wakuu na siyo kama watu wa chini
mbele ya matabaka mengine.
Mkurugenzi wa Shirika la CABUIPA Bw. David Rwegoshora akitoa ufafanuzi wa kina namna shirika lao linavyofanya kazi.
Ni
sahihi, kuona wananchi wakisimama imara, kujithamini na kujenga uelewa wa
misingi ya uchambuzi wa hali ya maisha yao. Lakini pia, kuwawezesha watu kuwa na
utamaduni wa kuthubutu kujaribu mambo mbalimbali ya maendeleo. Watu hao tunawaita
waraghbishi.Waraghbishi hawa wameanza uraghbishi tangu mwaka 2010 pale mpango
wa Chukua Hatua ulipoanza katika wilaya za Bukombe, Kahama, Shinyanga Vijijini,
Maswa, Kishapu na Bariadi. Ziliongezeka
wilaya mbili, Itilima na Mbogwe baada ya baadhi ya wilaya za Mkoa wa Shinyanga
kuhamishiwa mikoa mipya ya Geita na Simiyu na wilaya ya Ngorongoro kwa mkoa wa
Arusha. Uraghbishi ulianza kwa kikundi
cha watu wasiozidi 15 kupitia Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania
(MVIWATA) katika mkutano wa kimkakati uliofanyika katika Chuo cha Ushirika tawi
la Shinyanga, mwezi Septemba mwaka 2010. Miongoni mwao ni aliyekuwa Mwenyekiti
wa mtandao kwa Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Titus Ndugulile kutoka kijiji cha
Mwamala.
“Ni
vigumu kuamini kama mpango huu umekuwa mkubwa kiasi hiki. Tulianza watu 12 tu
miaka mitano iliyopita, lakini leo tupo waraghbishi zaidi ya 400. Kwa hakika
haya ni mafuriko ya waraghbishi, kwani sasa kila sehemu wanapatikana,” alisema
Ndugulile.Baada ya kikao hicho, yalifuata mafunzo maalumu ya uraghbishi kwa
siku tatu yakiendeshwa kila wilaya. Mafunzo hayo yalilenga kufundisha namna ya
kutafuta na kupata taarifa na kutambua changamoto zinazoikabili jamii na njia
za kuzitatua.
“Nilikwenda ofisi zetu za halmashauri kuulizia vyanzo
vya mapato vya wilaya na kuelezwa kuwa Mgodi wa Mwadui hauchangii chochote
pamoja na kuwa upo katika eneo hilo. Taarifa hii niliwashirikisha na wenzangu
pia.”Hayo ni maneno ya mraghbishi Fredina Said kutoka kijiji cha Negezi,
wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Pamoja na kwamba hakuweza kulifikisha mbali
suala hilo, angalau aliweza kufahamu kilichokuwa kikiendelea Pamoja na mambo
hayo, walifundishwa pia namna ya kujiamini kupitia mafunzo ya uraghbishi
waliyokuwa wakiyapata kwa mara ya kwanza.
Mafunzo haya yalitolewa kwa nadharia na vitendo ambapo
waraghbishi baada ya kupatiwa mafunzo ya darasani walipewa kazi ya kutembelea
ofisi za halmashauri za wilaya zao. Lengo
ni moja tu, kuwajengea uwezo wa kuongea na viongozi wa kitaifa kama mkuu wa
wilaya au mkurugenzi baada ya awali kuonyesha hofu na kutojiamini. “Ilikuwa
mara ya kwanza kuonana na mkuu wa wilaya na kumuulizia masuala ya pembejeo za
kilimo. Nilikuwa na hofu, hata hivyo kinyume na matarajio yangu, maswali yote
aliyajibu ingawa siyo kwa kiwango nilichotarajia,” alisema mraghbishi Fedson
Yaida wa Kijiji cha Shenda, wilaya Mbogwe, mkoani Geita Matokeo ya kutembelea
ofisi hizo yalionekana pale walipopatiwa majibu ya maswali yao.
Kazi hii ilikuwa na umuhimu mkubwa katika kuwandaa
waraghbishi na majukumu makubwa ya uraghbishi. Waraghbishi hawa walikuwa
wakiwakilisha wananchi wa vijiji vyao, hivyo moja ya jukumu lao ilikuwa ni
kuwashirikisha walichojifunza. Jukumu
hilo walilifanya vizuri na waliweza kutambuliwa kwa urahisi na viongozi wa
vijiji pamoja na wananchi wenzao. Na kwa sababu walipatiwa mafunzo kupitia
mradi wa Chukua Hatua, walijikuta wakiitwa kwa jina hilo hilo la Chukua Hatua.
Mfano mzuri ni waraghbishi waliopo katika kijiji cha Mwime, wilayani Kahama
mkoani Shinyanga.
Hali hii ilisababisha wananchi wengi katika vijiji ambavyo
mradi wa Chukua Hatua unaendeshwa kujitambulisha kama waraghbishi na kutaka na
wao wapatiwe mafunzo. Na hapo ndipo lilipokuja wazo la kuwawezesha waraghbishi
wa zamani na wapya kufanya kazi kwa pamojaAkielezea jinsi alivyowafundisha
waraghbishi jinsi ya kufanya uraghbishi katika kijiji chake na vile vya jirani,
mraghbishi kutoka Kijiji cha Ololosokwani, Kootu Tome, alisema: “Nimefundisha waraghbishi
wa kijiji cha jirani. Niliwaeleza maana ya uraghbishi, kwamba hawatakiwi kujionyesha
wazi kwa kila jambo, badala yake wanawashawishi watu kuchukua hatua katika kile
anachokuwa amewafafanulia,”
Viongozi wa mitandao ya
wilaya za Bukombe na Mbogwe mkoani Geita wakiwa katika kikao cha pamoja
kilichofanyika katika kata ya Masumbwe hivi karibuni
Mraghbishi
mwingine ni Julius Katende kutoka Kijiji cha Ngarwa, wilayani Ngorongongo
aliwafundisha waraghbishi wapya tofauti ya uraghbishi na uhamasishaji.
Mraghbishi si mwamasishaji, bali ni mtu anayeibua hoja katika jamii na
kuzitafutia majibu kwa kushirikiana na wenzake. Jumla ya waraghbishi wapya 762
wamefundishwa na waraghbishi 322 wa zamani, ikiwa ni ongezeko mara mbili katika
kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Julai hadi Septemba na kufanya idadi yao
kuwa 1,084. Kati yao, wanawake ni zaidi ya 400. Hili ni ongozeko kubwa ambalo
ni wazi linatokana na juhudi za pamoja. “Tuliwafundisha kutoka katika maeneo
mbalimbali ambayo wamekuwa na kawaida ya kukusanyika,” haya ni maneno ya mkurugenzi
wa Tamasha, Richard Mabala, wakati akifafanua namna wanavyoendesha mafunzo hayo
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Waraghbishi
kwa upande mmoja wanawakilisha wananchi wa maeneo yao na wamekuwa mstari wa
mbele kusimamia rasilimali zao na kuhakikisha huduma bora za jamii
zinapatikana. Lakini ili kufanikisha, malengo ya mpango wa Chukua Hatua,
viongozi wa vijiji, hasa wenyeviti, watendaji wa kata na vijiji wanafundishwa uraghbishi
pia kulingana na nafasi zao.Jukumu la kuwafundisha viongozi hawa kwa upande wa
mikoa ya kanda ya ziwa wamepewa CABUIPA, shirika mdau la mpango wa Chukua Hatua
lilipo Kahama. Akifafanua wanachofanya, mkurugenzi wa shirika hilo, David
Rwegoshora alisema:
“Katika
kipindi cha miezi mitatu tumefundisha wenyeviti 167 na watendaji 33 ngazi ya
kata. Kati yao, wanawake walikuwa sita.” Kwa upande wa Ngorongoro, wenyeviti
14, watendaji 14 wa vijiji na 6 wa kata walipatiwa mafunzo hayo. Kundi lingine
ni Sungusungu, ambapo hadi sasa idadi yao ni 15 nao walipewa mafunzo hayo ya
uraghbishi. Wote hawa ni waraghbishi kwa nafasi zao. Katika awamu iliyopita
ilijumuisha na viongozi wa dini wakiwamo masheikh, maimamu, wachungaji na
makatekista.
Katika
kuhakikisha waraghbishi wanawafikia watu wengi zaidi na kuwafundisha
uraghbishi, mitandao ya waraghbishi imeanzishwa katika wilaya za Mbogwe,
Kahama, Maswa, Kishapu, Bariadi, Shinyanga Vijijini, Itilima na Bukombe.
Mitandao hii ilianza rasmi mwaka 2014 na kuwaleta pamoja waraghbishi wa mikoa
ya Geita, Simiyu na Shinyanga. Hadi
sasa, kuna wenyeviti pamoja na wasaidizi wao, ambao idadi yao imefikia 32,
wanawake 16, sawa na asilimia 50. Wingi huu wa waraghbishi hauangalii itikadi
za vyama, badala yake unaangalia kilicho bora kwa wanajamii kwa ujumla.
<!--[if gte mso 9]>
0 comments:
Post a Comment