Kwa mara ya kwanza tangu Kamati Kuu ya CCM ilipomuengua kwenye kinyang’anyiro cha uspika, Samuel Sita ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, jana ameweka bayana mustakabali wake; ameamua kustaafu siasa.
Sitta
aliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe kirahisi
uenyekiti wa Bunge la Katiba na hivyo kujijengea jina miongoni mwa
wana-CCM kiasi cha kujitumbukiza kwenye mbio za urais na baadaye kutaka
kurudi tena kuliongoza Bunge la Kumi na Moja.
Lakini hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa angeengulkiwa angefika hata mahakamani.
Lakini jana alikuwa na kauli tofauti.
“Mambo
ya siasa kwa sasa basi,” alisema Sitta alipoulizwa na kuhusu mipango
yake ya baadaye baada ya kutopitishwa na CCM kuwania uspika.
Sitta
ambaye amewahi kuongoza wizara mbalimbali, alisema kwa sasa anajikita
katika uandishi wa vitabu na kwamba kwa umri alionao na utumishi wake
serikalini, umefika wakati kwake kupumzika na kutoa ushauri wa masuala
mbalimbali kwa wale watakaohitaji mchango wake.
Novemba
15, Kamati Kuu ya CCM ilimtosa Sitta na wengine waliojitokeza kuwania
uspika na badala yake ikateua majina matatu kwa ajili ya kupigiwa kura
na wabunge wa CCM, ambao walimchagua mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa
Spika.
Kuenguliwa
kwa Sitta kulikuwa ni pigo lake la pili katika nafasi ya hiyo baada ya
kukatwa na kikao hicho mwaka 2010 alipokuwa akitetea nafasi yake. Wakati
huo Anne Makinda alichaguliwa kuongoza Bunge la Kumi lililomaliza muda
wake mwaka huu.
Sitta
alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka 2005
hadi 2010, baada ya kuliongoza kuibua mijadala mbalimbali dhidi ya
Serikali na kashfa ya Richmond iliyomfanya Edward Lowasa kujiuzulu
uwaziri mkuu.
Baada ya kung’atuka
Alipoulizwa
atajishughulisha na nini baada ya kustaafu, Sitta ambaye pia alikuwa
mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alisema: “Nipo tu nyumbani
nimepumzika. Naridhika na niliyoyafanya kwa Taifa. Wale watakaotaka
kupata ushauri wakinifuata nitawasikiliza.”
Alisema
kwa sasa anaandika makala ambazo baadaye ataziweka katika kitabu chake
kitakachoeleza hali ya nchi na historia za masuala mbalimbali.
“Ninachokiandika ni mtazamo wangu binafsi, ni jinsi ambavyo mimi ninaona kwa macho yangu,” alisema.
Alipoulizwa
kama atakubali kuongoza wizara iwapo Rais John Magufuli atamteua kuwa
mbunge na kisha waziri alisema: “Tusizungumze jambo ambalo halina
mwelekeo huo.”
Hata hivyo, alisema kwa mtazamo wake hadhani kama anaweza kufikiriwa kuwamo katika baraza hilo.
Kupinga uspika kortini
Kuhusu
sakata la uspika, Sitta alisema angekwenda mahakamani kupinga
kuondolewa kwake, kama tu mchakato wa chama hicho ungefanyika bila
kufuata taratibu na watu kuonewa.
Katika
mazungumzo yake na Radio Uhuru FM wakati wa mchakato wa uspika, Sitta
alisema kutokana na hali ya joto la kisiasa ilivyo, ambayo ilidhihirika
zaidi wakati wa uchaguzi, wabunge walioshinda ni vijana na ni wazi spika
anayehitajika ni mwenye uzoefu.
Alisema
licha ya kwamba wapo waliojaribu kumshawishi asigombee nafasi hiyo
tena, badala yake awe anatoa ushauri pale inapobidi, alisisitiza bado
ana wito wa kuwatumikia wananchi kwa njia hiyo.
“Niliposema
(nitakwenda mahakamani) kama nisipoteuliwa na CCM kuwania uspika
nililenga kama kitatokea kitu kama uonevu. Yaani kama vingeletwa vigezo
ambavyo havipo katika mchakato,” alisema.
0 comments:
Post a Comment