Wafuasi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) wilayani Masasi, mkoa wa Mtwara wamechapana makonde
kufuatia mzozo wa kisiasa ulioibuka kati ya vyama hivyo.
Kufuatia vururugu hizo, polisi waliingilia kati na kufyatua risasi hewani kuwatawanya.
Wafuasi
hao walichapana makonde pamoja na kurushiana mawe jana katika maeneo ya
T.K, kwenye barabara kuu iendayo mjini Newala wakati walipokuwa
wakitoka katika mikutano ya kampeni ya wagombea wao wa ubunge
inayoendelea kwa ajili ya uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo.
Mashuhuda wa vurugu hizo wamesema kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya kundi la wafuasi wa UKAWA waliokuwa wakitoka
katika mkutano wa mgombea ubunge wa Cuf, Ismael Makombe, kwenye viwanja
vya Mti Mwiba alikokuwa akifanya mkutano wake na kurejea majumbani,
kukutana uso kwa uso na wafuasi wa CCM maeneo ya T.K ambapo walianza kuzozana juu ya sifa walizonazo wagombea wao.
Taarifa zaidi zinaarifu kuwa baada
ya mzozo huo wafuasi hao walianza kupigana na kurushiana mawe mazito
ikiwamo matofali na kupelekea baadhi kupata majeraha kwenye maeneo
mbalimbali ya miili yao na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa
matibabu.
Inaarifiwa kuwa
T.K ni kijiwe ambacho kinatumiwa na wafuasi wa CCM kukaa na kufanya
shughuli zao mbalimbali za kujiingizia kipato, lakini tangu kampeni
zianze hasa mikutano inapokuwa imeisha saa12:00 jioni, wafuasi wa Ukawa
wamekuwa wakipita eneo hilo huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kukibeza
CCM pamoja na mgombea wake Rashidi Chuachua.
0 comments:
Post a Comment