Msambatavangu anatuhumiwa na baadhi ya makada
wa chama hicho kukihujumu chama hicho jimbo la Iringa Mjini wakati wa Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu jambo walilosema limesababisha wapoteze kata 14 kati ya 18 na jimbo
hilo kwa mara nyingine tena kwa Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Wengine waliokutwa na kadhia hiyo ni
pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa
Iringa Elisha Mwampashi, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Yahaya Msigwa
na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa.
Wengine ni pamoja na aliyekuwa Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi
Kaskazini Mahamudu Mgimwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilolo, Joseph Muhumba.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika
kikaoni hapo kwa kuchelewa alijikuta akiingia katika kundi la wajumbe
waliofungiwa katika ofisi hizo baada ya kuwaomba vijana hao wafungue geti la
kuingilia na kutokea katika ofisi hizo zilizopo ghorofa ya kwanza ya jengo
hilo.
Baada ya kufungua geti hilo huku
wakimuahidi mkuu wa mkoa huyo kutoondoka katika ofisi hizo mpaka watakapojiua
nini kitafanywa na viongozi wa chama hicho kama mwenyekiti wa ccm mkoa wa
Iringa hataachia ngazi kwa hiari yake mwenyewe, walifunga tena geti hilo mara
tu baada ya mkuu wa mkoa kuingia katika ofisi hizo.
Wakiwa wamefungiwa ndani, makechelo wa
Polisi na wale Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa katika gari tatu za
polisi aina ya Landlover waliwasili katika ofisi hizo zilizopo jirani na stendi
kuu ya mabasi yaendeyo mikoani kwa lengo la kuwadhibiti vijana hao.
Baada ya askari hao kufika vijana
waliokuwa na funguo za geti hilo walipandisha harakaharaka ghorofani na kufungua
geti hilo kabla Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa na Katibu Mwenezi wake,
hawajatoka na kuzungumza nao.
“La kwanza niwapongezeni kwamba
mnakipenda chama na mnapenda chama kipate ushindi, pili niwapongezeni
mnauchukia usaliti ndani ya chama. Tatu lazima mfahamu kwamba kuna vikao
vinapaswa vijadili suala la usaliti, hoja yenu ni ya msingi,” alisema
Mwampashi.
Naye Dk Yahaya alisema uongozi wa chama
hicho mkoa umepokea taarifa za usaliti toka ngazi ya chini na mchakato wa
kuzijadili umeanza na akawaomba vijana hao kama wana nyongeza wawasilishe
katika kikao hicho cha kamati ya siasa ya mkoa.
Akizungumzia tuhuma wanazomuhusisha nazo
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa; mmoja wa vijana hao Salum Mbungu ambaye ni Katibu wa
Vijana Kata ya Ruaha na Katibu wa Makatibu wa Vijana wa kata zote 18 za jimbo
la Iringa Mjini alisema:
“Tunataka Mwenyekiti wa Mkoa ajiuzulu kwa
hiari yake, kuna ushahidi tosha unaomuhusisha yeye binafsi na baadhi ya vijana
wa CCM kukihujumu chama wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Mbungu alisema wanao ushahidi unaoonesha
kiongozi huyo alikuwa akiwashawishi baadhi ya wana CCM kuwachagua wagombea
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwasababu alikuwa mpiga
debe maarufu wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa wakati akiwa katika
mchakato wa kuwania urais kupitia CCM.
Akizungumzia tukio hilo baada ya vijana
hao kuombwa kutawanyika huku wakihakikishiwa kwamba hoja zao zinafanyiwa kazi
katika vikao husika, Msambatavangu alisema; “tuhuma zinazotolewa na vijana hao
na wana CCM wengine dhidi yake sio za kweli, zinalenga kuchafua hadhi yake na
kuficha ukweli wa sababu zilizosababisha wapoteze jimbo hilo.”
Alisema tuhuma zinazotolewa dhidi yake ni
za kupangwa na zinafanywa na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga kwa maslai
yake binafsi ili ashindwe kusimamia shughuli za chama kwa kuzingatia katiba,
kanuni na taratibu.
“Mimi siwezi kujiuzulu kwa shinikizo la
kikundi cha vijana wanaotumiwa vibaya. Tuna utaratibu wa kufanya tathimini za
uchaguzi, kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa; mkoa ukishachambua unapeleka Taifa
na maamuzi yanafanyika,” alisema.
Alisema wanaomtuhumu kwamba yeye ni
msaliti wanajua sababu nyingi, kwa kuwa zinajulikana, za kwanini walishindwa
uchaguzi katika jimbo la Iringa Mjini pamoja na kutumia nguvu kubwa.
Alisema anao ushahidi wa kina na wa
kutosha wa jinsi kiongozi mwenzake huyo wa mkoa anavyoratibu mipango ya
kumchafua kwa kutumia baadhi ya vijana hao ili kuficha ukweli huo.
“Nataka niwaambie watanzania wazaziwazi
kwamba kama mimi nilikisaliti chama eti kwasababu nilikuwa Timu Lowassa hiyo ni
hoja ya kipuuzi kabisa. Ndani ya CCM kuna demokrasia inayowapa fursa wanaCCM
kumuunga mkono mgombea wanayemtaka, na hiyo hawezi kusababisha sisi tuitwe
wasaliti, utaratibu huo upo toka enzi za Nyerere,” alisema.
Alisema wakati wa mchakato wa kutafuta
mgombea urais wa CCM, Lowassa aliungwa mkono na zaidi ya robo tatu ya wajumbe
wa halmashauri kuu, zaidi ya wenyeviti 16 wa mikoa na viongozi na wanachama
wengine mbalimbali kwasababu demokrasia hiyo inawaruhusu.
Alisema pamoja na Lowassa kuungwa mkono
na kundi kubwa alijitoa CCM na kujiunga na Chadema, waliomfuata walikuwa
wachache sana na hiyo haina maana kwamba waliobaki CCM ni wasaliti.
“Nimeanza kupigwa vita muda mrefu, na
vita hii ilianzia kwenye mchakato wa kupata mgombea ubunge jimbo la Iringa
Mjini kwasababu mimi nilikuwa mmoja wa wagombea ambaye nilipigwa vita na baadhi
ya viongozi, vita hiyo inaendelea kwakuwa mgombea waliyemtaka ameshindwa na
wanafanya hivyo wakitafuta kujikosha kwasababu waliwahakikishia wana Iringa
kwamba ni lazima watakomboa jimbo la Iringa Mjini,” alisema.
Alisema amepeleka taarifa makao makuu ya
chama ya jinsi anavyohujumiwa na kupakwa matope kwa tuhuma za uongo na kwamba
yupo tayari kutoa ushahidi wa kutosha pindi atakapotakiwa kufanya hivyo ili kusafisha
jina lake.
“Leo imefika mwisho, nataka niseme kama
mwenyekiti niliyechaguliwa na wilaya zote za mkoa wa Iringa; hujuma hizi zisizo
na ushahidi, hazivumiliki na zinachosha; nasema kama kuna mtu anatumia uongo,
uzushi na majungu kutaka mimi ning’oke, kabla sijang’oka Mungu atajibu,”
alisema.
Alisema hatishwi wala haogopi mipango
inayofanywa na vijana hao, na hata kama wana mpango wa kumua, wamuue, lakini
wajue historia itawahukumu kwasababu kazi anayofanya ya kukijenga chama hicho na
nguvu aliyotumia kwenye kampeni za CCM mkoa mzima kwa kutumia rasilimali zake
wanazijua.
Alisema inashangaza wanayemuita msaliti
(yeye) ilikuwaje wakamvumilia katika kipindi chote cha miezi miwili ya kampeni
na kuja kumutuhumu baada ya uchaguzi kufanyika na kupokeza jimbo.
“Inawezekanaje katika miezi miwili ya
kampeni, Jesca akaushinda uongozi mzima wa mkoa, uongozi wa vijana, uongozi wa
wanawake, uongozi wa wazazi, viongozi na wanachama wa kata na matawi, na
akavumiliwa katika kipindi chote hicho, kama hoja hizo sio za kipuuzi,”
alisema.
Alisema vijana hao wakiendelea kutumiwa
wajue kabisa kwamba hawatakuwa wanafanya kazi ya kukinusuru chama na akawataka
wakae chini, watafakari na wajipange upya kwa kutumia ngazi zote za chama
kujipanga upya.
Akizungumza
kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka Ludewa mkoani Njombe, Katibu wa
CCM mkoa wa Iringa, Mtenga alikanusha kuhusika na njama zinazodaiwa na
mwenyekiti wake huyo.
"Hicho
kikao wameitisha wenyewe, mimi sipo Iringa, ninawezaje kuhusika na
mambo yaliyokuwa yakiendelea katika kikao walichohitisha wao wenyewe,
sitendewi haki na kimsingi sina sababu ya kufanya hayo yanayodhaniwa
nayafanya," Mtenga alisema.
0 comments:
Post a Comment