Wednesday, December 23, 2015

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA AZUNGUMZIA KESI YA MWAKALEBELA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amesema anashangazwa na watu wanaomtuhumu kukihujumu chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu Jimbo la Iringa Mjini kwani madai yao hayana uhusiano wowote na sababu za msingi zilizotumiwa kufungua kesi ya kupinga matokeo ya jimbo hilo, hivikaribuni.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake juzi ikuwa ni siku tatu tu tokay eye na wajumbe wengine wa kamati ya siasa ya mkoa akiwemo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza wafungiwe ofisini kwa zaidi ya saa mbili, Msambatavangu alisema:

 “wakiwa barabarani wanasema Jesca alihujumu chama tukapoteza jimbo, lakini mahakamani hakuna mahali popote ambapo Jesca anatajwa kusababisha tupoteze ushindi huo.”

Alitoa ufafanuzi huo baada ya kumaliza kikao na baadhi ya vijana wa chama hicho walioahidi kuendelea kuwa watiifu kwake pamoja na uwepo wa shinikizo kutoka kwa wanachama wengine wanaoataka ajiuzulu kwa tuhuma za kutungwa.

Pamoja na kutoa ahadi hiyo ya utiifu, vijana hao walioongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Iringa, Kaunda Mwaipyana waliahidi kumpa ulinzi mwenyekiti huyo wa mkoa katika kipindi anachoendelea na wadhifa wake huo.

Akifafanua kuhusu tuhuma hizo, Msambatavangu alisema kama madai yanayotolewa dhidi yake yanaamini na baadhi ya wanaCCM wenzake; kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia chama hicho, Frederick Mwakalebelakwa vyovyote vile itapoteza uhalali.

“Vinginevyo wakabadilishe mashitaka ili kuhalalisha tuhuma zao dhidi yangu, maana kule mahakamani wanasema wamehujumiwa na Chadema na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo, lakini huku mitaani wananitaja mimi,” alisema.

Alisema tofauti na majimbo mengine ya mkoa wa Iringa, Iringa Mjini walijipanga vizuri kushinda uchaguzi huo kwa kuwa walikuwa na rasilimali fedha na watu ya kutosha, magari, pikipiki na vifaa vingine vingi vya kampeni.

“Badala ya watu kujiuliza jinsi rasilimali hizo zilivyotumika katika uchaguzi huo, watu wanazungumzia porojo zinazotungwa dhidi yangu na viongozi wenzangu ambao nilitofautiana nao mara tu baada ya kuonesha nia ya kutaka kuwania ubunge katika jimbo la Iringa Mjini, kabla ya kura za maoni za CCM,” alisema.

Alisema kura za maoni Jimbo la Iringa Mjini zilikuwa na ulaghai mkubwa kwani baadhi ya wanachama halali wa CCM wakiwemo wale wa muda mrefu walizuiliwa kupiga kura baada ya majina yao kwa makusudi kutoingizwa kwenye daftari la orodha ya wanachama.

Aliwataka wanahabari kupita katika kata mbalimbali za jimbo hilo ili kujionea ukweli huo ambao kwa kiasi fulani uliwakasirisha wana CCM ambao leo wakilaumiwa kwa matokeo ya uchaguzi jimbo hilo itakuwa ni sawa na kutowatendea haki.

“Iringa Manispaa lazima tujipange upya, tujifunze kuweka watu wanaokubalika na wananchi, sio wanaokubalika na viongozi. Watu walidhani wanapambana na mimi, kumbe wanapambana na wanachama wa mkoa mzima kwasababu wao ndio walioniamini wakanipa madaraka haya niliyonayo ambayo wengine hawataki niendelee kuwa nayo,” alisema.

Akizungumzia tukio la vijana wenzake kuifungia kamati ya siasa ya mkoa wa Iringa ofisini, Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Iringa, Kaunda Mwaipyana alisema kilichofanywa na vijana hao hakikubaliki na ni kinyume na kanuni za umoja huo.

“Kesho nitakuwa na kamati ya utekelezaji, tutapitia kanuni zetu ili tuone namna tutakavyowawajibisha vijana wote waliohusika katika tukio lile,” alisema.

Mbali na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Msambatavangu, wengine waliokutwa na kadhia ya kufungiwa ofisini na vijana hao ni pamoja na Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Elisha Mwampashi na Katibu Mwenezi wa Mkoa Dk Yahaya Msigwa.

Wengine ni  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa Ephraim Mhekwa, Godfrey Mosha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba.

Mwaipyana alisema moja ya jukumu kubwa la UVCCM kwa chama hicho ni kulinda usalama wa viongozi wake na sio kufanya kile kilichofanywa na vijana hao hata kama wana malalamiko kwani wanapaswa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu ili wanachokilalamikia kifanyiwe kazi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More