Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Bruno Kimaryo, kifungo cha miaka
miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza ujumbe katika
mtandao wa kijamii wa kuyapongeza majambazi yaliyovamia Kituo cha Polisi
cha Stakishari na kuua polisi. Aidha, mshtakiwa huyo ametakiwa ama
kulipa faini ya Sh. 600,000 kwa kosa hilo.
Katika
tukio la Stakishari lililotokea Julai 12, mwaka huu, majambazi
yalivamia kituo hicho na kuua polisi wanne na raia watatu pamoja na
kupora bunduki 20 aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema, baada ya
kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka.
Alisema vielelezo vitano na utetezi wa mshtakiwa vinaonyesha kuwa Bruno
alifurahia kitendo kilichofanywa na majambazi hao na alitamani kila
kituo cha polisi kivamiwe.
Alisema
mshtakiwa huyo katika ujumbe wake huo alitumia viunganishi vya maneno
yasiyokuwa ya kibinadamu ya auawe, avamiwe na kuwa utetezi wake
unaungana na maelezo ya onyo aliyoyatoa polisi hayaonyeshi kusikitishwa
wala kuhurumia polisi.
Hakimu
Lema alisema kama mshtakiwa angekuwa anapeleka ujumbe kwa polisi
wachukue tahadhari, angeupeleka katika mamlaka husika, lakini kutokana
na lugha aliyoitumia, mahakama hiyo inamtia hatiani.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kifungo.
Awali,
ilidaiwa kuwa Julai 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo
anadaiwa kusambaza machapisho ya uchochezi kinyume cha Sheria ya
Magazeti kwa nia kuleta ushawishi na kueneza chuki katika mtandao wa
kijamii wa facebook.
0 comments:
Post a Comment