Serikali
imesema mafunzo kwa ajili ya madiwani wote hayatakuwepo na badala yake
wenyeviti na makamu wa wenyeviti kote nchini ndio watapatiwa mafunzo ya
namna ya kusimamia halmashauri zao.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
anayeshughulikia Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jafo alisema hayo
wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo cha Serikali za Mitaa cha
Hombolo mjini Dodoma.
“Madiwani
ni wengi wote kuwapatia mafunzo haiwezekani kila halmashauri itatoa
mwenyekiti na makamu mwenyekiti, meya na naibu meya” alisema Jafo.
Alisema
mafunzo hayo yatahusisha wenyeviti wa halmashauri na makamu wao kutoka
halmashauri 185 nchini na kuwaagiza wakurugenzi kuhakikisha viongozi hao
wanafika Chuo cha Hombolo tayari kwa ajili kwa mafunzo hayo.
Alisema
miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu wa kuwapatia mafunzo madiwani
waliochaguliwa baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini sasa ni wenyeviti na
makamu wenyeviti wa halmashauri ndio watapatiwa mafunzo hayo.
Alisema
halmashauri 185 zilizopo nchini zitapeleka watu wawili kila halmashauri
na waliopata mafunzo hayo watakwenda kuwafundisha wengine.
Naibu
Waziri alisema kulikuwa na changamoto nyingi katika Uchaguzi Mkuu
uliopita na madiwani walichaguliwa kutokana na sifa zao na wengine
wananchi walifanya uchaguzi wa hasira, lakini mwisho wa siku kiongozi
aliyetakiwa alipatikana.
Alisema
madiwani wapya waliopatikana wapo wafanyabiashara, wanafunzi na watu wa
kada mbalimbali ambao wote walitakiwa kufundishwa namna ya kutenda kazi
zao.
Hata
hivyo, alisema mafunzo kwa ajili ya madiwani wote hayatawezekana, bali
viongozi wa madiwani hao ndio watapatiwa mafunzo hayo.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Dk Emmanuel Gibai
alisema maandalizi kwa ajili ya mafunzo hayo yamekamilika.
Awali
yalipangwa kutolewa kwa madiwani wote, lakini kutokana na maelekezo
hayo wahusika watakaotakiwa kupatiwa mafunzo hayo watayapata.
0 comments:
Post a Comment