Wakati
majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold
Corporation kuhusu wizi unaodaiwa kufanywa kwenye uchimbaji na
usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) yakiingia siku ya 64,
Ikulu imesema majadiliano hayo yanaendelea.
Majadiliano hayo yanafanyika kipindi ambacho Watanzania wengi wana shauku ya kuona rasilimali za madini zinanufaisha Taifa.
Katika
majadiliano hayo yaliyoanza Julai 31, timu ya Tanzania inaongozwa na
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Gerson Msigwa amesema majadiliano
yanaendelea na wananchi wasubiri wataelezwa kitakachojiri.
“Majadiliano
bado yanaendelea, wakiwa tayari watasema kwani hawawezi kuwa
wanajadiliana mara wanakwenda kusema katika media," amesema Msigwa.
Mazungumzo
hayo yalianza kufanyika kipindi ambacho Rais John Magufuli alikuwa
amekwishapiga marufuku ya kusafirisha nje makinikia hadi mgogoro wa
kimaslahi kati ya wawekezaji hao na Serikali utakapomalizika.
Miongoni
mwa kinachojadiliwa ni kodi ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imeitaka Kampuni ya Acacia kuilipa Serikali ya Tanzania Dola za Marekani
Bilioni 190 ambazo ni zaidi ya Sh 434 trilioni zinazodaiwa kutokana na
malimbikizo ya kodi na adhabu.
Msingi
wa mazungumzo hayo ni baada ya Rais Magufuli kuunda tume mbili
kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na wawekezaji hao
kwa zaidi ya miaka 19 iliyopita tangu walipoanza uzalishaji wa dhahabu.
0 comments:
Post a Comment