TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWA WOTE
WALIOOMBA KUTEULIWA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI NGAZI YA MIKOA NA TAIFA
Kwa Wana Jumuiya wote hususan wale
wote walioomba kuteuliwa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi kwenye UVCCM ngazi
ya Mikoa na Taifa. Kila mmoja anapaswa kuusoma, kujilinda, kuzingatia,
kuufahamu na kuuelewa ujumbe huu muhimu.
Zipo taarifa za uhakika zenye
vielelezo vyenye ushahidi kuwa baadhi ya walioomba nafasi za kuteuliwa kugombea
ndani ya UVCCM, wameanza kuitisha vikao vya mizengwe na kufanya kampeni za
chini kwa chini kinyume na Kanuni, Taratibu na mwenendo wetu wa Uchaguzi.
Ukusanyaji wajumbe kwa maana ya
wapiga kura katika eneo ambalo si halali kikanuni na kiutaratibu linatoa
tafsiri na kujenga mazingira ya rushwa pia ukiukaji na uvunjaji wa
kanuni za Uchaguzi za Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi.
Ifahamike kuwa uchaguzi huongozwa na
Katiba, Kanuni, Taratibu, miongozo na maadili halali hivyo kila mgombea anapaswa
kuheshimu taratibu hizo, sambamba na kuheshimu miiko ya uchaguzi.
Hadi sasa hakuna mwombaji wa nafasi
yoyote aidha wa nafasi ya Mkoa au Taifa aliyeteuliwa jina lake na kuwa mgombea
halali. Mamlaka za uteuzi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni hazijatangaza majina ya
wagombea walioteuliwa kutoka miongoni mwa waomba nafasi waliojaza fomu ndani ya
UVCCM.
Ni kosa na marufuku Kikanuni na
Kikatiba kwa muomba nafasi yeyote kuanza kupitapita Wilayani, Mikoani, mitaani,
vichochoroni, kuitisha vikao haramu vya kampeni , kujinadi na kujieleza kabla
ya ukamilishaji wa mchakato wa uteuzi na majina kutangazwa.
Vitendo vyovyote vitakavyofanywa
namuombaji wa nafasi aidha kwa kujinadi kwa kuitisha vikao haramu, kujielezea, kutaja malengo au kuwashawishi
wapiga kura kwa njia ambayo si ya kidemokrasia ni kinyume na taratibu. Ushahidi ukipatikana na
kuthibitika kunaweza kukuondolea sifa ya kuteuliwa katika nafasi
uliyoomba.
Tunaendelea kukumbusha kuwa
hatutasita kumchukulia hatua za kimaadili mpambe wa muomba nafasi yoyote
atakayebainika anakwenda kinyume na maelekezo haya pamoja na matakwa ya Katiba
ya Chama Chama Mapinduzi na Kanuni za UVCCM.
Hata baada ya vikao vya uteuzi kukamilika
mwongozo utatolewa kwa ngazi ya Mkoa hadi Taifa namna ya kufanikisha chaguzi hizo.
Chama Cha Mapinduzi ni baba na
kinara wa demokrasia Tanzania, Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla, chaguzi
hizi zinazoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake ni kielelezo tosha cha ukomavu
wa demokrasia na kioo kinachoakisi heshima ya Chama na Jumuiya ndani na nje
hasa katika kusimamia mambo yake ya msingi ya Kikatiba na Kikanuni.
Naendelea kuwakumbusha Vijana wote
kuendelea kuishi katika maneno ya Usia ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyowahi
kutuasa wakati chaguzi hizi zikiendelea nanukuu
“ Natambua mnaendelea na Uchaguzi ni lazima kuheshimu Katiba ya Chama chetu na Kanuni zetu katika
mchakato wa kuwapata Viongozi tutakaowapa dhamana. Vijana lazima wachague
Viongozi wazuri, wazalendo, waadilifu,
wachapa kazi watakaolinda maslahi ya CCM na UVCCM na si maslahi
binafsi kataeni na kupiga vita rushwa kwa nguvu zote na watakaobainika kutoa au
kupokea rushwa hatua za haraka zichukuliwe”; Dk. John Pombe Joseph
Magufuli.
Nachukua nafasi hii kwa sauti ya juu
kabisa kuwaonya, kuwaasa, kuwakanya na kuwazuia wale wote ambao aidha wanafanya
kwa makusudi au kujisahau waelewe kuwa Kanuni ya Uchaguzi iko pale pale na
itatenda haki kama msumeno. Vile vile watambue kuwa tunawamulika na kuwafuatilia
nyendo zao zote na ikibainika, taarifa zao zitawasilishwa katika vikao kwa
hatua zaidi za Kimaadili.
Ahsanteni
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu
Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
0 comments:
Post a Comment