Thursday, October 19, 2017

ALBAMU YA HAKUNA MATATA KUZINDULIWA OKTOBA 29 HIGHLAND HALL, IRINGA.

Mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka jijini Dar es salaam Dr. Tumaini Msowoya anawakaribisha wakazi wote wa Iringa na mikoa yote ya jirani katika uzinduzi wa albamu yake mpya iitwayo Hakuna Matata ikiwa ni albamu yake ya pili yenye mkusanyiko wa nyimbo nane ikiwemo Hakuna Matata, Amenitengeneza, Furaha, Mungu Mkuu, Wanawake, Mwamba ni Yesu, Samehe na Mungu wa Rehema, albamu hii itakuwa ikipatikana katika mfumo wa Audio CD.

Akiongea na gospomedia.com mwimbaji Dr.Tumaini Msowoya amesema kuwa uzinduzi huu utafanyika mjini Iringa katika ukumbi wa Highland Hall tarehe 29 Oktoba 2017 kuanzia saa nane mchana na kuendelea, Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa albamu hii ya Hakuna Matata atakuwa ni Mkuu wa wilaya ya Iringa Mh. Richard Kasesela ambaye atasindikizwa na wageni mbalimbali akiwemo Mchungaji Peter Msigwa ambaye pia ni mbunge wa Iringa na wageni mbalimbali wataohudhuria siku hiyo katika kumuunga mkono mwimbaji huyu.
Kwa upande wa huduma ya uimbaji Dr.Tumaini Msowoya amesema kuwa uzinduzi huu utapambwa na waimbaji na kwaya mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa, waimbaji watakaohudumu siku hiyo ni pamoja na Christopher Mwahangila, Ritha Komba, Witness Mbise, Tukuswiga IM, Stella Joel, Bahati Simwiche, Christina Mbilinyi, Moses Simkoko, Rebecca M, Matumaini, Bertha Mdemu na wengine wengi. Kwa upande wa kwaya zitakazohudumu siku hiyo ni pamoja na Kwaya ya Wakorinto wa pili(Mufindi), Kwaya ya Muhimidini vijana (Iringa Mjini) pamoja na kwaya nyingine nyingi ambazo pia zitakuwa baraka katika kuusindikiza uzinduzi wa albamu hiyo.

Kuhusiana na yeye kufanya uzinduzi wa albamu hii mkoani Iringa Dr.Tumaini msowoya amesema kuwa ”Ninafanya uzinduzi huu mkoani Iringa kwa sababu wao ni sababu ya hatua zangu zaidi…. Dar nina muda mfupi sana tangu nihamie kwa hiyo nimeona nirudi Iringa kuwarudishia kile walichonituma watu wangu wa nguvu…..”
”Hakuna Matata ndiyo wimbo unaobeba jina la albamu yangu mpya na huu ni wimbo unamuongezea mtu nguvu kwamba hata kama kuna jaribu gumu kiasi gani, kushinda ni lazima. Ukiwa na Yesu hakuna matata. . ..Kuna wakati majaribu huwa yanaumiza moyo cha msingi ni kujipa moyo. ..kutokata tamaa na kusonga mbele”. Alimaliza na kusisitiza Dr.Tumaini Msowoya na kuwasihi wakazi wote wa mkoani Iringa na mikoa ya jirani kufika siku ya uzinduzi albamu hiyo ili kumtia moyo katika kufanikisha safari yake ya kulitangaza neno la Mungu kupitia nyimbo za muziki wa Injili.

Kabla ya kuhamia jijini Dar es salaam Dr.Tumaini Msowoya alikuwa akifanya kazi kama mtangazaji wa redio ya Ebony Fm na baadae kuwa mwenyekiti wa vijana (UVCCM) wa mkoani hapo.
Mbali ya kuwa mwimbaji wa muziki wa Injili, Dr. Tumaini Msowoya kwasasa pia ni mwandishi wa gazeti (Mwananchi) na ni mwanaharakati wa ukombozi wa wanawake nchini Tanzania.
Kwasasa anafanya vyema na wimbo uitwao Furaha ukiwa ni moja ya wimbo unaopatikana kwenye albamu hii mpya ambao hata wewe utakwenda kukubariki na kubadilisha maisha, Karibu usikilize na upakue wimbo huu na usiache kufika siku ya uzinduzi wa albamu ya ”Hakuna Matata”


DOWNLOAD AUDIO

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More