Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula
Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alipotembelea banda la Kampuni ya POLYTECH MACHINERY inayojishughulisha na uuzaji wa mashine mbalimbali ikiwemo za kukamua mafuta ya alizeti wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula
Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita. Mwingine ni Mhe Dkt Mary Mwanjelwa Naibu waziri wa Kilimo (Kulia).
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula
Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula
Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Na Mathias
Canal, Geita
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba leo
Octoba 16, 2017 amefunga rasmi maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula
Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita kuanzia
Octoba 10 mpaka Octoba 16, mwaka 2017.
Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho hayo waziri Tizeba alisema
kuwa Kuanzia msimu huu wa kilimo Wakulima wa korosho
watapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.
Alisema Hatua hiyo ni
utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha vikwazo vyote
vilivyokuwa, vikiwakabili Wakulima wa
zao la korosho vinaondolewa ili kuwawezesha kuongeza uzalisha na tija zaidi
kutokana na zao hilo.
Mhe Tizeba alisema Madhumuni ya Maadhimisho
ya Siku ya Chakula Duniani ni kutoa nafasi ya kutafakari, namna Jamii katika
ngazi ya Kaya, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa zinavyoweza kuhakikisha ongezeko la
uzalishaji na upatikanaji wa chakula cha kutosha na chenye lishe bora kwa watu
wote na kwa wakati wote.
Alisema kuwa Kila mwaka Shirika la Chakula Duniani (FAO)
baada ya kufanya tathmini ya hali ya Chakula hutoa Kaulimbiu ambayo huwa ni
dira ya maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.
Kaulimbiu ya mwaka huu 2017 inasema “Badili mwelekeo wa uhamaji; Wekeza katika
usalama wa chakula na maendeleo Vijijini”. Kaulimbiu hii inaweka umuhimu katika kuweka Mipango na
Programu zinazolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo
Vijijini; kupuza utegemezi na kuongeza usawa katika Jamii, sambamba na uhifadhi
mazingira ambayo ndiyo muhimu katika maendeleo ya kilimo na hifadhi ya Jamii
ili yachochee jitihada za kuondoa umaskini.
Alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani
kwa mwaka huu ni ya kujivunia kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, kwa kipindi
chote nchi yetu imejitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100 na hivyo
kuwa na ziada ya chakula.
Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2016/2017 umefikia
Tani 15,900,864 za chakula kwa
mlinganisho wa nafaka. Kati ya kiasi hicho, tani 9,388,772 ni za mazao ya nafaka na tani 6,512,092 ni za mazao yasiyo nafaka.
Hata hivyo Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2017/2018
yatakuwa Tani 13,300,034 ambapo Tani 8,457,558 ni kwa mazao ya nafaka
na Tani 4,842,476 ni mazao yasiyo
nafaka.
Dkt Tizeba aliongeza kuwa Kutokana na uzalishaji huu,
nchi itakuwa na kiwango cha utoshelevu wa asilimia
120 ambapo kiwango hiki kinaonyesha kuwa nchi itakuwa na ziada ya chakula
ya Tani 2,600,831 ambapo mazao ya
nafaka kutakuwa na ziada ya Tani 931,214
na mazao yasiyo nafaka ni Tani 1,669,617
kwa viwango vya utoshelevu vya asilimia
111 na 134 mtawalia. Alisema
Ziada hii inatosha kwa matumizi ya chakula hapa nchini na kuwa na ziada ya
kuuza.
Katika hatua nyingine Mhe waziri wa kilimo ametumia fursa
hiyo kuwaasa wananchi wote kuwa na hifadhi ya chakula katika kaya zao na
kutumia chakula kilichopo kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.
‘‘Wahenga walisema usione vyaelea
vimeundwa; hivyo mafanikio tuliyoyapata ni matokeo ya jitihada za Serikali,
Wadau, Wabia wa Maendeleo na Wananchi wote kwa ujumla wao kwa kuendelea
kushiriki katika shughuli za maendeleo hususani kilimo, ufugaji, uvuvi na
huduma mbalimbali zinazotolewa, Aidha
zipo changamoto mbalimbali zikiwemo,
mabadiliko ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa
uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji
lakini Tumejipanga kuendelea, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya
tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazovumilia ukame,
magonjwa na kutoa mavuno mengi” Alisema Mhe Dkt Tizeba
Sambamba
na hilo, alisema kuwa serikali imejipanga kuendelea kuwaelimisha na kuwasaidia
Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalamu zaidi ili kuepuka ile hali ya kuhamahama
kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.
Kilele
cha maadhimisho ya siku ya Chakula Dunia ilihudhuriwa na Makatibu Wakuu, Makatibu
Tawala, Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mwakilishi
wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi
wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji, Viongozi wa Vyama vya Siasa, na Viongozi
wa Dini.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment