Monday, October 23, 2017

WALIMU WA SHULE YA KWAKILOSA WANAKAA KWENYE MAWE NA MAGONGO KUANDA MAANDALIO YA KUFUNDISHIA

 Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati akiongea na wanafunzi,wazazi na walimu wakati wa mahafali ya kidato cha nne mwaka huu 2017 katika shule ya sekondari ya Kwakilosa iliyopo katika manispaa ya Iringa 
Baadhi ya wanafunzi na wazazi walihudhuria sherehe za kuhitimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Kwakilosa iliyopo kata ya Mwangata.



Na Fredy Mgunda,Iringa.


Shule ya sekondari ya kwakilosa iliyopo kata ya Kwakilosa manispaa ya iringa inakabiliwa na upungufu wa madawati na viti vya walimu na kusababisha kudorola kwa elimu katika shule hiyo.

Akizungumza wakati wa mahafali ya shule hiyo mkuu wa shule Hudson Luhwago alisema kuwa walimu wanafanya kazi za wanafunzi katika mazingira magumu kutokana na ukosefu wa viti na meza za kufanyanyia kazi.

“Walimu wangu wa shule hii wanakaa kwenye mabanzi au juu ya mawe kutokana na uhaba wa viti hivyo hatuwezi kupata elimu bora maana maandalio yote yanafanyika mahali ambapo sio salama” alisema Luhwago

Luhwago aliongeza kuwa shule hiyo inaupungufu wa madawati takribani mia moja hivyo kusababisha wanafunzi kusoma wakiwa kwenye msongamano mkubwa kwenye dawati moja hivyo wanafunzi wanapoteza usikivu kwa walimu.

“Wanafunzi wengi wanashindwa kupata elimu iliyobora kutokana na kukosekana na madawati na ndio chanzo cha utoro wa wanafunzi katika shule hii hivyo wanafunzi huwa wanakuwa na furaha kipindi cha mitihani kwa kuwa halarusiwi kukaa wawili wawili” alisema Luhwago

Aidha Luhwago aliwatupia lawama uongozi wa kata ya kwakilosa kwa kutotoa ushirikiano kwa walimu juu ya kutatua changamoto ambazo zinawakabili wanafunzi na walimu wa shule hiyo.

“Niliwahi kupeleka changamoto hivi kwa viongozi wa kata na wakanijibu hawana muda saizi wanashughulikia swala chama sasa hapo ndio utakapogundua kuwa kazi ya ualimu ni ngmu” alisema Luhwago

Luhwago aliwataka wanasiasa kuondoa siasa kwenye vitu ambavyo sio vya kisiasa kwa kuwa kushuka kwa ufaulu wa shule ya sekondari ya Kwakilosa kunasababishwa na wanasiasa.

Akisoma risala mbele ya mgeni makamu mkuu wa shule ya Kwakilosa Praygod Makonwa alisema kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa viti 45 na meza 45 kwa walimu jambo linalosababisha walimu kukaa kwenye mawe na magogo na kushindwa kuandaa vipindi kwa waledi unaotakiwa.

Makongwa alisema kuwa shule hiyo inaupungufu wa majengo ya utawala,kukosekana kwa maktaba,maabara ya masomo ya sayansi,ukosefu wa nyumba za walimu kunachangia kushuka kwa elimu katika shule hiyo.

Kwa upande wake mgeni rasmi ambaye ni mbunge wa viti maalum mkoa wa iringa kupita chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati alisema kuwa atawachangia viti ishirini katika awamu ya kwanza na baadae atatoa meza.

“Kwa leo ngoja nianze na kuwachangia huo mchango wangu mdogo nilionao maana hii shule inachangamoto nyingi za kuzitatua naombeni walimu msikate tamaa juu ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenu kwa kuwa hawa ndio taifa letu la sasa” alisema Kabati

Kabati aliwataka wazazi kuendelea kuchangia maendeleo kwa faida ya watoto wao wanaosoma katika shule hiyo na kuondokana na mazingira magumu ambayo wanakumbana nao walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

“Mimi ni mdau wa maendeleo ndio maana nimekuwa nikitoa msaada sana kwenye sekta ya elimu na afya ili kuwafanya wanafunzi wa mkoa wa iringa wawe wa mfano kwa kupata elimu bora na kuwa mfano kwa wananchi wa Tanzania” alisema Kabati

Kabati alitoa kompyuta moja kwa ajili ya maendeleo ya wanafunzi ili waendane na sayansi na teknolojia iliyopo kwa sasa ambayo ndio inasaidia kuleta maendeleo kwa haraka zaidi.


“Jamani achene siasa maendeleo hayana siasa hivyo naomba tufanye maendeleo kwa ajili ya watoto wetu na familia zetu,siasa muwaachie wanasiasa maana wao hawaumii kama nyinyi mnavyo umia” alisema kabati

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More