Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya utakatishaji fedha na
kugushi inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey
Nyange ‘Kaburu’ hadi October 11, 2017 kwa sababu upelelezi
haujakamilika.
Mwendesha
Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu,
Godfrey Mwambapa kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na
upelelezi haujakamilika, hivyo anaomba ipangiwe tarehe nyingine ambapo
baada ya kueleza hayo Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi October
11, 2017.
Evans
Aveva na Makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya
kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani
300,000.
Katika
shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya
kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakionesha
Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans
Aveva wakati si kweli.
Katika
shtaka la pili alidai kuwa March 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la
Azikiwe Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka ya uongo ambayo ni fomu ya
maombi ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakati akijua ni kosa.
Katika
la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya
March 15 na June 29, 2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya
kutakatisha fedha kwa kupata Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua
ni zao la uhalifu.
Kwa
upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati
ya March 15, 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za
kimarekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika
shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa
March 15, 2016 katika benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia
Aveva kujipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo
zimetokana na kughushi.
Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
0 comments:
Post a Comment