Monday, April 23, 2018

BAADA YA UJENZI WA MAGHALA NA VIHENGE VYA KISASA KUKAMILIKA (NFRA) ITAKUWA NA UWEZO WA KUHIFADHI TANI 501,000

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba akitoa taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi huo Mtaa wa Relini-Kizota Mjini Dodoma, Jana 21 Aprili 2018. Picha Na Mathias Canal-NRFANa Mathias Canal, NFRA-Dodoma

Hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini inazidi kuimarika huku serikali kupitia wizara ya kilimo ikiwa imejipanga kukabiliana na changamoto ya uchache wa maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali hususani mahindi.

Katika taarifa ya Bi Vumilia L. Zikankuba Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula katika hafla ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kisasa katika Mtaa wa Relini-Kizota Mjini Dodoma aliyoitoa mbele ya mgeni rasmi-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) jana tarehe 21 aprili, 2018 alieleza kuwa mradi huo pindi utakapokamilika utafungua fursa kubwa kwa wakulima nchini.Alisema kuwa Baada ya Mradi huu kukamilika uwezo wa kuhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Kuhifadhi Chakula utakuwa mara mbili ya uwezo wa sasa yaani kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000 huku ikitarajiwa kufikia Tani 700,000 kufikia mwaka 2025.

Bi Vumilia alieleza kuwa Mikataba ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula, ilisainiwa na kuanza kazi tarehe 09 Desemba 2017 kati ya (NFRA) na makampuni mawili toka nchini Poland ambayo ni Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o. Aidha, mradi huo utatekelezwa kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 55 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi kumi na nane (18) kuanzia mwezi Mei 2018.

Maandalizi ya awali ya mradi huo yalifanywa na kampuni kutoka nchini Poland iliyofanya upembuzi yakinifu wa awali na kupendekeza gharama za mradi kuwa dola za kimarekani millioni 55 ambazo zingetosheleza kujenga vihenge vyenye uwezo wa Tani 150,000 na maghala yenye uwezo wa Tani 50,000, hivyo kufanya uwezo wa jumla wa mradi kuwa Tani 200,000.

Alisema, ili kujiridhisha zaidi Wakala kupitia Wizara mama, iliunda timu ambayo ilifanya upya tathmini ya mradi na kupata thamani halisi ya mradi (value for money) ili kuleta ushindani katika utekelezaji wa mradi kwa kushirikisha timu ya Wataalamu wa ndani.

Timu hiyo iliundwa na Wahandisi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi na Wataalamu wa mazingira kutoka TBA pamoja na Mhandisi toka Wizara ya Kilimo. Hivyo timu hiyo ilifanya upya kazi ya usanifu wa msingi, kuandaa makadirio ya gharama za mradi, na kuandaa makabrasha ya zabuni ili kutimiza azma mbili nilizotangulia kuzitaja hapo awali.

Matokeo ya jumla ya kazi hiyo, yalibainisha kuwa kiasi cha fedha Dola milioni 55 kinatosheleza ujenzi wa vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 190,000, na maghala Tani 60,000 hivyo kufanya ongezeko la hifadhi ya Tani 50,000.

Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unamiliki maghala ya kuhifadhi nafaka 34 yenye uwezo wa jumla ya Tani 251,000. Uwezo huu wa sasa wa maghala hautoshelezi mahitaji ya dharula ya chakula kwa mfululizo wa miezi mitatu kwa akiba isiyo pungua Tani 700,000, hivyo kupelekea uhitaji wa kuongeza uwezo wa uhifadhi.

MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More