Rais John Magufuli amewatoa hofu wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhusu
uteuzi wao kwa kuwataka kuchapa kazi kwa bidii ili wawe na nafasi nzuri
ya kuteuliwa badala ya kufanya kazi kwa wasiwasi jambo ambalo matokeo
yake yatakuwa kuondolewa.
Dk Magufuli alitoa kauli hiyo juzi
kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Chato mara baada ya kutua kwa
helikopta akitokea Mwanza kuelekea nyumbani kwake Kijiji cha Rubambangwe
kwa mapumziko.
Akiwahutubia mamia ya wananchi waliokuwa
wamefurika uwanjani hapo, Dk Magufuli alisema anatambua kuwa bado
hajachagua wakuu wa wilaya na wakurugenzi hali ambayo imewafanya baadhi
yao kuwa na wasiwasi na kushindwa kutekeleza majukumu inavyotakiwa.
“Kama wewe ni mchapakazi mkuu wa wilaya, mkurugenzi una wasiwasi gani?
Tena unapokuwa na wasiwasi ndivyo uwezekano wa kung’olewa unakuwa
mkubwa,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na kuongeza:
“Lazima
niwaambie waheshimiwa wakuu wa wilaya, ukiwa na wasiwasi hutafanya kazi
na sisi tunakuona tu unafanya kazi kwa wasiwasi utaondoka tu kwani
wasiwasi ni dalili nzuri ya kukufanya uondoke.”
Aliwatoa hofu
akisema hata watakaoondolewa kwenye nafasi hizo watapangiwa kazi
nyingine lakini akawaambia kwamba hata kama wataondolewa wasihofu kwani
haitakuwa mbaya kwa kuwa hawakuzaliwa na ukurugenzi au ukuu wa wilaya.
Alisema
Watanzania wanatakiwa kumwamini na kurudia kauli yake kwamba
hatawaangusha akiahidi kuondoa kero ambazo zimegeuka mzigo kwa wananchi.
“Wako wengine walianza kulalamika natumbua mno majipu, siyo
kutumbua tu ikiwezekana kuna mengine nitayakata kabisa na mguu wake,
Tanzania lazima iwe yenye neema, haiwezekani kuwa na wafanyakazi 5,000
wanaolipwa mishahara mikubwa halafu Watanzania milioni 50 wanalia…
nitakwenda kujibu nini kwa Mungu,” alisema.
Alisema ataendelea
kuwatumbua (kuwawajibisha viongozi wazembe) hata kama wanafika 50,000
ilimradi Watanzania milioni 50 wapate neema ya kufaidika na rasilimali
yao.
Alisema watu katika nchi hii wanaishi bila raha na
kuwaahidi kuwa itapatikana kwa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii hasa
vijana na kuacha tabia ya kucheza pool huku mama zao wakienda shambani
kulima na kusubiri kula tu.
0 comments:
Post a Comment