Katika kile kinachoonekana kutaka kuliongoza Jiji la Dar es Salaam kwa
mafanikio ya kupigiwa mfano, Chadema imeunda chombo kipya cha uongozi
katika jiji hilo na kukiita ‘Uongozi wa Dar es Salaam Kuu’.
Pia, imemteua Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuwa mwenyekiti wa chombo hicho.
Chama
hicho kikuu cha upinzani nchini kimeunda chombo hicho, huku kikieleza
kuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi wa meya wa jiji hilo kwa
ushirikiano na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ikilinganishwa na CCM.
Uchaguzi
huo umeahirishwa mara tatu na ya mwisho kwa kutumia zuio ‘batili’ la
Mahakama na kuzua mtafaruku kati ya wabunge na wadiwani wa chama hicho
dhidi ya polisi, jambo lililosababisha wabunge wawili, Halima Mdee na
Waitara pamoja na madiwani watatu kufikishwa mahakamani wakidaiwa
kumshambulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando
ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo.
Akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu jana,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema katiba ya chama hicho
iliubadilisha Mkoa wa Dar es Salaam kuwa mamlaka ya kichama ya kimkoa na
hivyo wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke zimepewa jina la mkoa badala
ya wilaya.
“Baada ya kuona sintofahamu ya uchaguzi wa meya na
namna ambavyo Serikali inavifanyia vyama vinavyounda Ukawa kuhusu suala
hilo, chama kiliunda uongozi wa kimkoa, kimeamua kujipanga upya katika
Jiji la Dar es Salaam,” alisema Mbowe.
Alisema wameunda chombo
hicho kwa mujibu wa Ibara ya 6.1.3 ya katiba ya chama hicho ili
kurejesha demokrasia iliyopotea katika Jiji la Dar es Salaam.
Ibara hiyo
inasema; Kwa kuzingatia ibara ya 6.1.2, ngazi ya juu ya chama itateua
kamati ya muda itakayokuwa na wajibu wa kuratibu shughuli za chama na
kuwaunganisha wanachama katika eneo lisilo na uongozi wa kikatiba mpaka
watakapofikia uwezo wa kuwa na uongozi wa kikatiba.
Alisema
kifungu hicho kinaongezewa nguvu na kifungu cha katiba cha 7.5.1
kinachoeleza jinsi ngazi za uongozi zinavyoundwa katika kila eneo la
mkoa wa kiutawala wa Serikali Kuu, “Katika ngazi hii patakuwa na mikoa
ya chama ambayo imetimiza masharti yaliyobainishwa na katiba na sehemu
(c) inasema wilaya za Dar es Salaam zitakuwa na hadhi sawa ya kimkoa ya
chama.”
Mbowe alisema mikoa hiyo ya kichama ya Kinondoni, Ilala
na Temeke, itakuwa na chombo kitakachoiunganisha ambacho ni uongozi wa
Dar es Salaam Kuu.
“Uongozi huo umeteuliwa makusudi ili kuongeza nguvu,
usimamizi na uratibu wa operesheni za chama katika jiji hili,” alisema.
Alisema chombo hicho kitakuwa na wajumbe wasiozidi 25 na uongozi wa
chama hicho katika mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala utabaki vilevile.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kamati inayounda chombo
hicho itawahusisha wabunge wote wa kuchaguliwa na wa viti maalumu wa
Chadema mkoani humo na mameya wa Ilala na Kinondoni.
Wabunge hao ni Mdee, John Mnyika (Kibamba), Waitara, Saed Kubenea (Ubungo), Susan Lyimo, Anatropia Theonist na Lucy Mollel.
Wengine
ni mgombea wa Chadema katika nafasi ya umeya wa Jiji, Yesaya Mwita,
Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob
pamoja na baadhi ya madiwani na viongozi wengine wa chama hicho jijini
Dar es Salaam akiwamo Henry Kilewo ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa.
“Mwenyekiti
wa kamati hii atakuwa Waitara na Makamu wake ni Bernard Mwakyembe
ambaye ni diwani kutoka Wilaya ya Temeke. Katibu atakuwa Kilewo na Mweka
Hazina ni Lyimo,”alisema Mbowe.
0 comments:
Post a Comment