Watu watatu wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi na ujambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Watu hao walikutwa na karatasi yenye ujumbe kwa aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ulioandikwa:
“Nasaha kwa Kova, mzee andaa kamati ya mazishi ya vipolisi vyako tukiwamaliza tutakufikia wewe.”
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa tukio hilo,
lilitokea Jumamosi iliyopita, eneo la Fire, jijini Arusha wakati
mtuhumiwa Athumani Kassim alipokamatwa eneo la Engosheraton akiwa na
silaha na aliwataja wenzake.
Kamanda Sabas alisema walipopata
taarifa kutoka kwa raia wema walio tilia shaka mwenendo wa mtuhumiwa
huyo ambaye alipokamatwa, alikutwa na milipuko, makoti makubwa mawili na
kofia ya kuficha uso.
“Baada ya mahojiano, alituambia kuna wenzake wawili anashirikiana nao kufanya uhalifu na tuliweka mtego.
“Saa
5 usiku, askari wetu wakiwa wameambatana na Kassim, walipofika jirani
kabisa na nyumba hiyo eneo la Fire, alitoa ishara na wenzake wakaanza
kuwashambulia polisi kwa risasi,” alidai kamanda huyo.
Hata hivyo, Sabas alisema polisi waliwazidi nguvu na kuwajeruhi wawili kati yao.
Hata hivyo, magaidi hao walimpiga mwenzao risasi na wao walifariki dunia walipokuwa wakipelekwa hospitali.
Alisema
kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, walikuta vitu mbalimbali ikiwamo
sare tano za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kofia tano za kuficha
nyuso, vazi moja la karate, pikipiki moja iliyobomolewa na imebandikwa
namba bandia.
Alivitaja vitu vingine kuwa ni bendera mbili nyeusi zenye maandishi ya Kiarabu zinazotumiwa na makundi ya kigaidi.
Vitu
vingine ni kisanduku cha chuma na hati ya kusafiria ya Abrahaman
Athuman Kangaa, iliyotolewa Aprili 2, 2013, simu tano za mkononi na kati
ya hizo, moja ilitambulika kuwa ni ya marehemu Mary Joseph aliyefariki
kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Februari 20, mwaka huu, eneo la
Engosheratoni pamoja na kifurushi cha unga wa baruti na jambia moja.
Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya utambuzi.
0 comments:
Post a Comment