Msichana
wa umri wa miaka 17 ambaye alikuwa katika machungu ya uzazi, amejikuta
akijifungulia mtoto chooni baada ya muuguzi mmoja wa Hospitali ya Amana
jijini Dar es Salaam kumtaka aende kuoga na kubadilisha nguo bila ya
kujali hali yake.
Msichana
huyo, Asha Sudi (17), mkazi wa Tabata Kisiwani, alikutwa na tukio hilo
juzi wakati akisubiri kujifungua, na uongozi wa Amana umesema
utalishughulikia suala hilo.
Asha alisema alifika hospitalini hapo saa 4:00 asubuhi akiwa anaumwa na uchungu na alipofika mapokezi alikalishwa kwenye benchi.
“Wakati
nikiwa nimekaa kwenye benchi alikuja nesi akaniambia niende chooni
nikaoge na kubadilisha nguo. Kwa sababu sikujua, nikaenda,” alisema Asha.
Alisema
akiwa chooni anajiandaa kuoga, uchungu ulikata ghafla na baada ya
dakika chache aliona kitu kinaning’inia sehemu za siri kisha kikadondoka
chini.
Baada
ya kuona hivyo, alianza kupiga kelele akiita “nesi, nesi” na ndipo
alipopita wa kwanza ambaye hata hivyo hakumshughulikia na badala yake
akaendelea na kazi zake, lakini baadaye akaenda daktari ambaye
hakumtambua kwa jina, akamsaidia.
“Nikiwa ninatapatapa sielewi alikuja daktari akamuokota mtoto ambaye alikuwa ameanguka chini karibu na tundu la choo,”alisema.
Baadhi
ya wauguzi walitoa ushuhuda wa tukio hilo, wakiwamo daktari aliyemuokoa
mama huyo na mwanaye chooni, lakini hawakutaka majina yao yatajwe
“Nilikuwa
wodini. Wakati napita nikasikia mtu anapiga kelele chooni akiita ‘nesi,
nesi, mwanangu jamani’. Nilishtuka, ikabidi niende kuona ndipo
nikamkuta huyo binti akiwa amesima na kondo likiwa limening’inia na
kitoto kichanga kimeanguka chini,” alisema.
Alieleza kuwa alikiokota kichanga hicho na mama yake kisha kuwapa huduma ya kumsafisha mtoto.
Muuguzi
mwingine ambaye alikuwa zamu mchana, alisema alipopita kumuangalia
mtoto huyo, alikuta akiwa na uvimbe kwenye paji la uso.
“Nikamuuliza
mama wa mtoto ndipo akanisimulia. Kwanza nikashangaa huyu nesi
ilikuwaje akamruhusu mama ambaye anataka kujifungua kwenda chooni?” alihoji.
Mkuu
wa Idara ya Wazazi, Grace Massawe alisema wamelichukua suala hilo na
kwamba watalishughulikia, lakini akawataka wazazi na ndugu wa mama huyo
kuwa watulivu na kuwasamehe waliofanya tukio hilo.
“Mama
tumekuelewa hili suala tutalishughulikia. Aliyefanya kosa hilo
tutamuita. Najua alijisahau hasa ukizingatia bado ni mgeni, lakini
tutalifanyia kazi,” alisema.
Mkuu
wa Idara ya Mama na Mtoto wa hospitali hiyo, Francis Kioweli alisema
mtoto huyo hajapata athari ya kiafya na kwamba endapo kutatokea tatizo
lolote, basi wazazi hao wasisite kwenda hospitali kwa uangalizi zaidi.
0 comments:
Post a Comment