Monday, March 28, 2016

20 Watiwa Mbaroni Wakituhumiwa Kumpiga Mawe Ofisa wa JWTZ

Polisi mkoani Ruvuma inawashikilia waendesha bodaboda 20 Manispaa ya Songea wanaodaiwa kumshambulia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 411 KJ Ruhuwiko, kwa kupiga mawe gari alilokuwa akiendesha baada ya kumgonga mtembea kwa miguu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zubeir Mwombeji alisema tukio hilo lilitokea Machi 24 saa 3.00 usiku maeneo ya Shule ya Msingi Mfaranyaki, karibu na Kituo Kikuu cha Polisi Songea Mjini.

Mwombeji alimtaja mwanajeshi huyo aliyejeruhiwa kwa kushambuliwa na waendesha bodaboda kuwa ni Luten Samweli Nginila (32), ambaye amelazwa Hospitali ya Rufani Mkoa.

Alisema Luteni Nginila alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na kupoteza fahamu baada ya kushambuliwa na waendesha bodaboda, ambao walivunja kwa mawe vioo vya gari alilokuwa akiendesha.

Aliendelea kuwa chanzo cha tukio hilo, inadaiwa kutokea ajali maeneo ya majengo ambako askari huyo alikuwa akiendesha gari aina ya Nissan XTRAIL akitokea Bar ya Ramour .

Alisema alipofika eneo la majengo, Bahati Mbero alikatisha ghafla barabarani hivyo askari huyo kushindwa kumudu gari na kusababisha ajali.

Kufuatia hali hiyo, waendesha bodaboda waliokuwa karibu walikusanyika kwa lengo la kumshambulia, hali iliyomlazimu kuwasha gari kukimbia ili kuokoa maisha.

Hata hivyo, bodaboda hao walimkimbiza na alipofika Shule ya Msingi Mfaranyaki tairi la gari lake lilichomoka, hivyo walimzingira na kumshushia kipigo wakiwamo abiria watatu aliokuwa nao.

Mwombeji aliwataja waliokuwamo ndani ya gari hilo kuwa ni Kaumbya Kateka (24) mkazi wa Majengo, Joyce Edson (24) mkazi wa Mpambalyoto na Jackline Mwita (22) mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Peramiho. Alisema katika vurugu hizo baadhi ya vitu vilipotea ambavyo ni mali ya askari huyo.

Vitu vilivyopotea ni simu mbili za mkononi, pochi ambayo ilikuwa imehifadhi vitambulisho mbalimbali na Sh120,00.

Alisema wanaendelea kuwabaini wengine waliohusika, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafuata.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More