Na Fredy Njeje-Blogs za Mikoa
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Anna
Mghwira amesema umiliki wa ardhi kwa wanawake hapa nchini bado unasuasua
kutokana na mfumo dume uliopandikizwa tokea miaka ya nyuma.
Bi Mghwira ambaye alikuwa mwanamke pekee
aliyegombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015 kupitia
ACT Wazalendo, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Blogs za Mikoa kuhusu sababu
za wanawake wengi nchini kutomiliki raslimali muhimu ya ardhi.
Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 idadi ya
wanawake hapa nchini ni asilimia 51% lakini wanaomiliki ardhi ni
asilimia 19% tuu jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa wanawake wengi bado
hawamiliki ardhi ukilinganisha na wanaume.
''Tatizo lililopo hapa nchini ni tatizo la
kitamaduni, ilikuwa kazi ya mwanamke akishazaliwa ni alelewe na baadaye
akiolewa anaendeleza kizazi huko alikoolewa lakini kumiliki ardhi ni
mfumo mpya ambao unatoa fursa sawa katika kumiliki raslimali hiyo muhimu
kwa ajili ya kuitumia katika shughuli za kiuchumi''Amesema Mghwira.
Bi Mghwira ameenda mbali zaidi na kuona
tatizo la umiliki wa ardhi pia lipo kwa upande wa wanaume hasa
inapotokea suala la makubaliano na mwekezaji ndiyo maana kuna kesi
nyingi kuhusiana na wawekezaji na wananchi katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
Baadhi ya wanaume waliopo katika mmoja ya Kijiji Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wakiongea na Blogs za Mikoa kutoa maoni yao ya namna ambavyo walikuwa hawakubaliani na wanawake kumiliki Ardhi
Katika jitihada za kuunga mkono Serikali
katika jitihada mbalimbali za kutatua kero kwa wananchi Bi Mghwira
amesema kwamba mara kwa mara amekuwa akielimisha wanawake hapa nchini
katika kutambua haki zao na kujikwamua na umasikini.
Hata hivyo ameitaka serikali kutizama upya
sheria ya ardhi na pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umiliki wa
ardhi ili kuwezesha wananchi kutambua kuwa umiliki wa ardhi ni wa haki
kwa pande zote kwa upande wa wanaume na wanawake.
0 comments:
Post a Comment