Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)
na DW, Salma Said amedai alitekwa na wanaume wawili baada ya kumkamata
na kumuingiza kwenye gari lao kisha kuondoka naye na kumpeleka
kusikojulikana.
Salma aliyetekwa Ijumaa iliyopita na watu hao
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea
Zanzibar kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake kwenye moja ya hospitali za
jijini Dar, alisimulia mkasa huo jana mbele ya waandishi wa habari huku
akimwaga machozi.
Alisema alipoteremka uwanjani hapo, alimpigia simu dereva wake amfuate na wakati akimsubiri, ndipo wakatokea watu hao.
Salma
alisema watu hao walimfunga mtandio wake mweusi usoni ili asibaini
mahali walikokuwa wakimpeleka na kumfungia chumbani .Alisema ndani ya
chumba hicho kulikuwa na vitambaa.
“Waliponiingiza ndani ya
chumba kile siku ya kwanza, wakanifungua tambala usoni kwa hivyo
nikawaona nyuso zao, mmoja alikuwa na kovu shavuni, mrefu na mwingine
mweupe kidogo, waliniweka kule ndani bila kupata chakula chochote,”
alisema.
Salma alisema alitakiwa kurudi Zanzibar kwa ajili ya
kuripoti marudio ya Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika juzi, lakini
alishindwa baada ya watu hao kumteka na kumfungia kwenye chumba hicho.
Alidai kuwa watu hao walimwambia watamuachia baada ya uchaguzi huo kufanyika na mgombea wa CCM kutangazwa kuwa mshindi.
Katika
mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Baraza
la Habari Tanzania(MCT), Salma aliongozana na Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Katibu Mtendaji wa MCT,
Kajubi Mukajanga na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu Bara (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, ambao kwa pamoja walieleza
kupinga ukatili huo huku wakiliomba Jeshi la Polisi kuwasaka wahalifu
waliohusika.
“Walinisababishia maumivu makali, walinipiga mabuti
na makofi huku wakiniambia maneno ya vitisho kama ilivyokuwa kwa Dk
Ulimboka na Kibanda,” alidai Salma.
Kabla ya watekaji hao
kumrudisha katika eneo walilokuwa wamemteka, Salma alidai kuwa watu hao
walimpiga kila walipoingia na kutoka nje ya chumba alichowekwa na
kumsababishia apumue kwa tabu.
Akijibu swali la mwandishi wa
habari aliyetaka kupata ufafanuzi wa taarifa za uvumi wa kujiteka
mwenyewe, Salma alijibu swali hilo huku akidondosha machozi: “Hakuna
sababu ya kusema uongo, mimi ni Mwislamu na dini yangu inakemea kufanya
hivyo.”
Pia, alisema amefanya kazi kwa miaka zaidi ya 20 na
matukio ya vitisho yalianza alianza kuyapata muda mrefu kwa kupigiwa
simu, kutumiwa meseji na kufuatwa nyumbani kwake.
Salma ambaye
alizungumza huku akionyesha ushahidi wa meseji za makundi ya mitandao
yanayojadili kufurahishwa na kutekwa kwake, alisema kujiteka ni kauli
zisizokuwa na uhusiano wowote na ukweli, kwani alijitambulisha kuwa
mwandishi mtetezi wa haki za binadamu na siasa ambazo zinazokinzana na
maslahi ya wachache.
Wakati huohuo; Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema ni mapema kuzungumzia tukio
la kutekwa kwa Salma kwa madai kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment