Mbunge wa Kinondoni, (CUF), Maulid Mtulia amepinga mpango wa walimu wa
Mkoa wa Dar es Salaam kusafiri bure kwenye daladala akisema utawashushia
heshima.
Badala yake, alitaka Manispaa ya Kinondoni iweke
utaratibu wa kuwaongezea walimu fedha za usafiri kwenye mishahara yao
ili wajilipie wenyewe.
Kauli ya mbunge huyo imekuja baada ya
Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Paul Makonda kutangaza kuwa walimu wa shule za
Serikali za Dar es Salaam watasafiri bila kulipa nauli kwenye daladala.
Katika
mpango huo ambao umepangwa kuanza Jumatatu ijayo unaozigusa pia
manispaa za Temeke na Ilala, walimu watapatiwa vitambulisho maalumu
vyenye saini ya Makonda.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
juzi, Mtulia alisema licha ya kuwa wazo lililenga kuwasaidia walimu,
lakini litawasababishia dhihaka.
Alisema kinachopaswa kufanyika
ni kutafuta suluhisho la kudumu la kero zinazowakabili walimu ambazo
zinachangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
“Itafika hatua
kondakta atamsimamisha mwalimu kwenye kiti kama ilivyo kwa wanafunzi
kwa sababu tu halipi nauli… Wazo hili ni zuri lakini lilipaswa
kuboreshwa kama kweli nia ni kumsaidia mwalimu,” alisema.
Alisema ikiwa
kweli nia ni kuwasaidia walimu, basi halmashauri zina wajibu wa kuhesabu
siku za kazi na kiasi ambacho mwalimu atalipia nauli ili fedha hizo
ziongezwe kwenye mshahara wake.
Alisema njia hiyo itakuwa ya
heshima zaidi kuliko walimu kusafiri bure kwa kutumia vitambulisho kama
walivyo wanafunzi wao.
Hata hivyo, alisema ipo haja kwa viongozi wa
manispaa hiyo kukaa meza moja na walimu ili kujua changamoto
zinazohitaji suluhu ya haraka, akisema huenda nauli ikawa si ya msingi
kwao.
0 comments:
Post a Comment