Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Freeman Mbowe,
amewashauri Watanzania wasife moyo kwa matokeo mabaya ya uchaguzi
yaliyopinduliwa; na kwamba matokeo hayo yawe chachu ya kufanya vizuri
zaidi katika uchaguzi ujao.
Amesema uchaguzi si tukio, bali mchakato; na kwamba kama kuna watu wamekufa moyo kwa sababu ya kilichofanywa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupindua matokeo, hasa ya urais, watafakari upya na wajipange kwa kazi kubwa inayokuja, kwani mafanikio ya kisiasa hayapimwi kwa tukio moja la uchaguzi na matokeo yake. Alisema matokeo hayo yanapswa kuwatia hasira na kuwahamasisha waendelee kupambana,
Mbowe aliyasema
hayo Masaki, nyumbani kwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa Zamani ambaye
pia alikuwa Mgombea Urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye hafla ya
kumshukuru Mungu iliyoandaliwa na familia hiyo. Ukawa unaundwa na
Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
“Hatukushinda
serikali kuu kama tulivyokusudia na kupenda iwe kwa sababu ambazo si
wakati wake kuzisema sasa, lakini ni vema tukumbuke kwamba mapambano
tunayofanya, kama kuna yeyote miongoni mwetu anafanya kwa ajili yake
binafsi, ana wajibu wa kujitafakari upya,” amesema Mbowe.
Aliongeza
kwamba, kazi ya mapambano wanayofanya viongozi sasa ina manufaa kwa
kizazi kijacho, na kama wanaoifanya sasa wakafanikiwa kuonja matunda ya
kazi ya mikono yao basi ni jambo la kumshukuru Mungu.
“Kazi
anayofanya Lowassa (Baba Kadeti) si lazima aone matunda yake leo,
huenda mtoto wake ataonja na asipoonja Kadeti basi wajukuu wataonja
matunda hayo na kutambua mchango mzuri wa babu yao kwa kazi kubwa ya
maana anayofanya sasa,” amesema.
Aliwahimiza
Watanzania zaidi ya 600 waliokuwepo kwenye halfa hiyo kuwa wale walio
wafuasi wa vyama vya siasa hata wasio na vyama wana wajibu wa kuendelea
kwa nguvu zote na kazi ya kupambana ambayo Lowassa amejiunga nayo, kwani
wakati wa uchaguzi watu wengi walipigana kumsaidia sio kwa ajili ya
familia yake ila walifanya vile kwa sababu ya nchi hii, huku Lowassa
akiwa kiongozi na mpeperusha bendera.
Mbowe
alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania waendelee kumwombea neema,
ujasiri na afya njema Lowassa kwani taifa bado linamhitaji kuliko
pengine anavyohitajika na familia yake.
Aidha,
Mbowe alimsifu pia Regina, mke wa Lowassa, kwa ujasiri wake na familia
nzima kwa uamuzi mzuri na ujasiri aliochukua katika kuhakikisha
Watanzania wanatafuta haki na ujasiri kwa kukata minyororo ya watesi.
“Mama
ulikuwa mwoga kwenye kampeni katika hatua za awali, lakini baadaye
ulipata ujasiri kama mgombea mwenyewe. Asante sana kwa kuondoa woga;
asante kwa kuongoza familia, na sasa tuendelee na mapambano.” alihimiza Mbowe
Kabla
ya Mbowe kusimama, neno la kuwashukuru watu waliofika nyumbani
lilitolewa na Regina akasema familia, hasa Lowassa mwenyewe, ilikuwa
inasubiri kwa hamu siku ya kumshukuru Mungu na Watanzania kwa mazuri
mengi aliyowatendea.
Hafla
hiyo ya shukrani ilianzia kwa ibada katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, Dar es Salaam. Lilichagizwa na
nyimbo kadhaa za shukrani zilizopendekezwa na Lowassa mwenyewe, na
kuimbwa na washiriki wote, wakiwamo wa madhehebu mengine ya dini.
Miongoni
mwa washiriki wa hafla hiyo ni baadhi ya wanachama wapya wa UKAWA
waliojiengua CCM mwaka jana, wakiwamo Hamisi Mgeja, Mgana Msindai,
Lawrence Masha, John Guninita, na wengine.
Ilihudhuriwa
pia na wanasiasa, viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali, vijana na
wazee, matajiri na watu wa kawaida kutoka sehemu mbalimbali.
“Tumepata
mengi mazuri, tunaweza kusafiri kwenda Monduli na kurudi si sababu tuna
magari mazuri kuliko wengine; tunaweza kusafiri kwa ndege na tukarudi
salama, lakini hata wakati mwingine unasikia mtu anakupigia simu
kukusalimu au kukuandikia ujumbe mzuri wa faraja, haya yote ni sababu
ya Mungu na tukaona leo tufike Kanisani kusema Mungu asante kwa mema
yote uliyotujalia,” alisema Regina akiwa amejawa tabasamu muda wote, huku akishangiliwa.
Wajukuu
wa Lowassa walijumuika kumwimbia babu yao wimbo kutoka miongoni mwa
tenzi za Injili zilizoandaliwa kwa ajili hiyo, huku wakiongozwa na mpiga
kinanda.
Baada
ya wajukuu, Masha alitumbuiza washiriki kwa wimbo wa Kiingereza
“Amazing Grace,” akatuzwa kiasi cha Tsh. 50,000 ambacho, hata hivyo,
alikigawa kwa wajukuu wa Lowassa.
0 comments:
Post a Comment