Sunday, March 6, 2016

Ikulu Yavunja Ukimya Sakata la Umeya Dar

 
Ikulu imevunja ukimya kuhusu ile sinema ya kuahirishwa mfululizo kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kusema haitaona tatizo lolote iwapo Halmashauri hiyo itaongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Uchaguzi huo utakapofanyika na vyama hivyo kushinda na kuongoza Jiji, Ikulu imesema, hakutaathiri hata kidogo shughuli zake za kila siku hivyo haina mkono wake kwenye sarakasi za uchaguzi huo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, alipoulizwa  ni kwanini Ikulu isiingilie kati na kuamuru kufanyika kwa uchaguzi huo ambao umeshapigwa danadana muda mrefu.

“Hilo la hisia kwamba Ikulu ina mkono wake kwa kuhofia Ikulu kuwa chini ya Ukawa si kweli hata kidogo,” alisema Balozi Sefue.

 "Sisi tuogope nini wakati wao hawataathiri shughuli zetu za kila siku? Nakuhakikishia hatuoni tatizo lolote."

Kumekuwa na tetesi kwamba serikali inahofia upinzani kuchukua Jiji, kwani Ikulu ni kama itakuwa ndani ya eneo linalotawaliwa na wapinzani hali itakayoleta mgongano wa kiutendaji na kimaslahi.

Balozi Sefue alisema Jiji kuongozwa na Ukawa hakuwezi kuwanyima usingizi hata kidogo kwasababu iko miji mingi mikuu duniani ambayo inaongozwa na vyama vya upinzani na shughuli za Ikulu kwenye miji hiyo zinaendelea kama kawaida.

“Sisi hatuhofii na wala hatuoni sababu ya kuingilia uchaguzi huo ati kwa kuhofia Ukawa kuongoza Jiji, mbona miji mbalimbali duniani inaongozwa na vyama vya upinzani na mambo yanakwenda kama kawaida?" Alihoji.

"Sisi hatutakuwa wa kwanza duniani na wala hakuna kitakachobadilika.”

Kuhusu zoezi hilo kutawaliwa na ubabaishaji, Balozi Sefue alisema kwa sasa Ikulu haiwezi kuingilia kati na kulazimisha siku ya uchaguzi huo kwasababu wahusika wapo na hawajasema kama wameshindwa.

“Waziri anayehusika na Tamisemi yupo na hasema kwamba ameshindwa. Sasa kwanini sisi tuingilie suala lao?

"Mimi naamini hawajashindwa na wakishindwa wenyewe wanajua waende wapi kwa ajili ya ufumbuzi.

Mvutano wa Umeya wa Jiji umetokana na vyama vinavyounda Ukawa kuvuna madiwani wengi kuliko CCM katika jiji la Dar es Salaam hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kutwaa Halmashauri ya Jiji, ikiwa uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru na haki.

Jiji lina madiwani 76 wa CCM wakati Ukawa ina 87.
Tayari Halmashauri mbili kati ya tatu za Dar es Salaam zinaongozwa na Ukawa: Ilala na Kinondoni wakati CCM ikiongoza Temeke pekee.

Hata idadi ya wabunge kwa Dar es Salaam, Ukawa imeizidi kwa mbali CCM ambayo imepata wabunge wanne tu ambao ni Faustine Ndungulile wa Kigamboni, Issa Mangungu (Mbagala), Bona Kaluwa (Segerea) na Mussa Azan Zungu (Ilala).

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana Ukawa ilichukua majimbo ya Kawe linaongozwa na Halima Mdee (Chadema), Ukonga la Mwita Waitara (Chadema), Ubungo la Saed Kubenea (Chadema), Kibamba la John Mnyika (Chadema) na Kinondoni la Maulid Mtulia (CUF).

Katika kuonyesha kuwa sakata hilo bado ni moto, madiwani na wabunge wanaotoka Ukawa, juzi walivamia ofisi za Jiji wakishinikiza waambiwe tarehe ya uchaguzi huo.

Wanachama hao wa Ukawa walikaa kwa saa nzima kwenye ofisi hizo bila kupata jibu kutoka kwa wahusika na walisikika wakilaumu uongozi wa Jiji kuwa umepanga kuwahujumu.

Ingawa Ikulu ilisema kuwa haiwezi kuingilia suala hilo kwa kuwa Waziri husika hajashindwa, kuna dalili kwamba waziri mwenye dhamana amenawa mikono na hajui namna ya kutatua tatizo hio

Jiji liko chini ya Tamisemi ambayo iko Ofisi ya Rais hivyo kumekuwa na hofu kwamba iwapo Ukawa watachukua kiti cha Meya, kutakuwa na mgongano mkubwa wa sera na utekekelezaji wa ilani ya upinzani na ya Ukawa.

Vyama vya Ukawa vilishatoa angalizo hivi karibuni kwamba serikali inajaribu kutengeneza mgogoro ili kumpa nafasi Rais John Magufuli kuvunja Halmashauri ya Jiji na kuunda tume ya jiji.

Sheria ya Tamisemi ya mwaka 1982 inampa mamlaka Rais kuvunja Halmashauri ya Jiji/Mji/Manispaa na kisha kuteua tume.

Mwaka 1996, Fredrick Sumaye, akiwa Waziri Mkuu, aliivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuunda tume iliyoongozwa na Charles Keenja.

Wiki iliyopita ziliibuka vurugu za kurushiana makonde kati ya wafuasi wa Ukawa na Polisi kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi huo kutokana na madai ya kuwepo zuio la muda Mahakama lilowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambalo baadaye ilibainika kwamba lilikuwa feki.

Kabla ya wiki iliyopita, uchaguzi wa Meya wa Jiji ulishaahirishwa mara moja kwa sababu za kiujanja ujanja kutokana na pingamizi la CCM.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More