Polisi mmoja anadaiwa kumpiga risasi dereva daladala, Pistus Ngowi baada ya kutofautiana kauli.
Tukio
hilo lililotokea juzi saa tatu usiku, Kariakoo jijini Dar es Sallam
lilisababisha madereva wenzake wanaofanya wote safari za Tandika pamoja
na wa Temeke kugoma kwa zaidi ya saa tano wakidai kwamba licha ya
kushambuliwa, amebambikiwa kesi katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Ilidaiwa
kuwa wakiwa katika Mtaa wa Lindi kilipo kituo cha daladala hizo, polisi
huyo aliyetajwa kwa jina moja la Dotto akiwa kwenye doria,
walitofautiana na dereva huyo kisha kumtolea bastola na kumpiga nayo
mkononi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon
Sirro alisema jana kuwa awali, alipewa taarifa za askari wake
kushambuliwa akiwa doria na alimpiga risasi dereva huyo kujitetea.
“Huyu askari yupo mahabusu anahojiwa na polisi ili kubaini chanzo cha tukio hili,”alisema Kamanda Sirro.
Dereva
wa daladala aliyeshuhudia tukio hilo, Mateso Elias alidai kuwa walikuwa
madereva 15, waliokuwa wakisubiri abiria ghafla walisikia kelele za
Dotto akimfokea dereva huyo akidai kuwa alitaka kumgonga alipokuwa
akiwasili kituoni hapo.
Alisema ili kuepusha shari, Ngowi
alishuka kwenye basi na kumuomba msamaha akiwa amepiga magoti lakini
polisi huyo alikataa kumsamehe.
Alisema kitendo hicho kiliwavuta
madereva waliokuwapo hapo ambao walisogea eneo hilo kujua kilichokuwa
kinaendelea: “Ghafla alitoa bastola na kutuamuru wote tuondoke.
Tulipopiga hatua kama hatua tano, alifyatua risasi na kumpiga Ngowi
mkononi na nyingine alipiga hewani.”
Alisema baada ya tukio hilo aliwapigia simu askari wenzake ambao walifika na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
0 comments:
Post a Comment