Monday, March 21, 2016

Maalim Seif Afunguka wakati Wazanzibar wakipiga Kura.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alitangaza kususia uchaguzi wa marudio licha ya jina lake kujumuishwa kwenye makaratasi ya kura, amesema ameiachia CCM kuamua hatma ya nchi hiyo.

Akiongea jana katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam alipotembelewa na Wajumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), wakati uchaguzi wa marudio ukiendelea visiwani Zanzibar, Maalim Seif alisema kuwa CCM ndio walitengeneza hali iliyopo hivi sasa na kwamba ndio wanajua hatma ya uamuzi huo.

“Mimi sijui [hatma ya Wazanzibar], wauliezeni CCM wao ndio wametengeneza hali hii… wao ndiyo wamekusudia na wanajua wanaipeleka wapi nchi hii,” alisema Maalim Seif.

“Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM ambao pamoja na kwamba wanafahamu mshindi ni nani katika uchaguzi wa mwaka jana, wameamua kufanya hicho walichofanya hivi sasa,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais amesema kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha alitumiwa na CCM kufanya maamuzi na kwamba uamuzi huo umerudisha nyuma maridhiano yaliyofikiwa miaka mitano iliyopita.

Alisema kuwa hivi sasa hatazungumza kitu chochote hadi pale matokeo ya uchaguzi wa marudio yatakapotangazwa lakini akasisitiza kuwa Wazanzibar wanajua mioyoni mwao Rais wao ni nani.

Jana wananchi wa Zanzibar wamepiga kura katika uchaguzi wa marudio kufuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana. 

Amani na utulivu vilitawala katika uchaguzi huo ulioshuhudia kuwepo kwa ulinzi mkali.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More