Watumishi
watatu wa Ghala la Taifa la Hifadhi Chakula wamesimamishwa kazi,
wakidaiwa kuchanganya kwa makusudi mahindi mabovu na mazuri na
kuwapelekea wananchi.
Uamuzi
huo ulichukuliwa mjini Arushajana na Naibu Waziri wa Mifugo, Kilimo na
Ushirika, William Ole Nasha baada ya kufanya ziara kwenye ghala mkoani
hapa.
Waliosimamishwa
kazi kupisha uchunguzi ni Meneja Brightone Mollel ambaye ni msimamizi
mkuu wa ghala na maofisa wawili kutoka Makao Makuu Dar es Salaam ambao
ni Dunia Mlokozi na Silvano Mwakinyela.
Wanatuhumiwa pia kuuza mahindi hayo ya serikali kwa wafanyabiashara mbalimbali mkoani Arusha na nje ya nchi.
Imedaiwa kutokana na vitendo hivyo, wamejinufaisha na kuwa mamilionea huku wananchi wakinyanyasika kwa kula chakula kibovu.
Hata
hivyo, Meneja huyo, Mollel alimweleza waziri kuwa tuhuma zinazoelekezwa
kwake si za kweli, kwani hajawahi kufanya unyama huo wala kuuza mahindi
ya serikali.
Akifafanua
kwa waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya ghafla katika ghala
hilo, Naibu Waziri Nasha alisema hujuma ya kuwalisha watanzania chakula
kibovu, imefanyika kwa miaka mingi na amekuwa akipata malalamiko mengi
mkoani Arusha na nje ya mkoa.
Nasha
alisema serikali haiwezi kuwaachia kirahisi watumishi wa aina hiyo
wenye uchu wa utajiri kwa kuwaangamiza wananchi kwa maslahi yao.
Alikielezea kitendo hicho kuwa si cha huruma.
Kwa
mujibu wa naibu waziri huyo, mahindi mabovu ambayo yametengwa,
huchanganywa na mahindi mazuri na kusambazwa kwa ajili ya matumizi ya
binadamu huku wahusika wakijua wazi kuwa hayafai kwa matumizi hayo.
‘’Angalia
ubovu wa mahindi haya, lakini vigogo wa ghala hili wakishirikiana na
wafanyabiashara, wanachanganya na mahindi mazima na kisha wanapeleka
wilayani kwenye uhaba wa chakula.
"Wananchi
wamekuwa wakilalamika kila mara kuwa mahindi yanayopelekwa huko hayafai
kuliwa na hata na mbuzi au ng’ombe hawali, hali iliyonifanya kufuatilia
kwa karibu na kuja kujionea mwenyewe bila kuambiwa,’’ alisena Nasha.
"Hawa watu nimewasimamisha kazi kuanzia leo (jana) mpaka uchunguzi upite ni kwa nini wanafanya hivyo, hii haikubaliki,’’ alisema Nasha.
Baadhi
ya wafanyakazi wa ghala hilo na wabeba mizigo, walikiri kwamba hali ya
kuchanganya mahindi mabovu na mazuri iko katika ghala hilo kwa muda
mrefu na wamekuwa wakilazimishwa kufanya hivyo kwa maslahi ya baadhi ya
watumishi.
Mmoja
wa wafanyakazi hao, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema watendaji
hao wakuu wa ghala, wana utajiri mkubwa unaohusishwa na hujuma hiyo ya
mahindi.
“Kuna
kigogo mmoja alimpa mtoto wake wa kike zawadi ya gari V8 VX yenye
thamani ya zaidi ya Shmilioni themanini siku yake ya kuzaliwa. Baadhi ya
watumishi wa serikali katika ghala hili wanaishi kama wapo peponi kwa
kuwapa watanzania chakula kibovu.
"Mahindi ya serikali huuzwa na mengine kusafirishwa nchi jirani ya Kenya bila ya kubughudhiwa,” alisema mfanyakazi huyo. Mfanyakazi mwingine alisema kuna mtandao mkubwa wa kuuza mahindi ya serikali.
"Kibaya
zaidi watanzania wanalishwa chakula kibovu chenye hatari kwa afya huku
wao wakijitajirisha kwa mahindi mazuri yanayoenda nje ya nchi kwa njia
za panya," alisema mfanyakazi mwingine aliyeomba jina lihifadhiwe.
Alisema, "Naomba
Waziri unilinde kwani ninaweza kuuawa, hata nikifukuzwa kazi sioni
tatizo, lakini roho inauma sana ninapoambiwa nichanganye mahindi mabovu
yenye sumu na mahindi mazuri ili yakaliwe na watanzania, hiyo ilituuma
sana wabeba mizigo wote’’.
Alisema
malalamiko hayo waliyafikisha ofisi ya mkuu wa wilaya siku nyingi
kuelezea hujuma hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu alikiri
kuwa na taarifa hiyo na alisema ndio maana amekuja na waziri husika,
anayeshughulika na sekta hiyo.
Nkurlu
alisema pia Waziri mwenyewe amekiri kupata malalamiko katika wilaya za
Karatu, Ngorongoro na Simanjiro kuwa mahindi ya misaada yanayopelekwa
huko, hayafai kuliwa na binadamu kwani hata mifugo inakataa kula.
0 comments:
Post a Comment