Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, Rosemary
amewaomba radhi Watanzania kwa kauli yake kwamba Olduvai Gorge iko
nchini humo.
Rosemary alisema hakuwa na nia mbaya alipotoa kauli
hiyo, bali aliitoa kwa bahati mbaya akimaanisha eneo jingine lililoko
Kenya linaloitwa Olorgesalile.
Alifafanua kuwa matamshi hayo hayakulenga kupotosha ukweli, bali ulimi uliteleza.
Katika maelezo aliyotoa kupitia akaunti yake ya Facebook, Rosemary aliandika:
“Habari
za jioni. Nimekuwa nikikumbushwa kuhusu tukio lililotokea wakati
nahudhuria kongamano la vijana New York, miezi saba iliyopita.
Niliteleza ulimi kwani sikumaanisha Olduvai Gorge badala yake nilitaka kumaanisha Olorgesalile,” alisema na kuongeza:
“Nawapa
pole Watanzania kutokana na usumbufu uliojitokeza, kaka zangu na dada
zangu poleni sana na Olduvai Gorge yenu bado iko salama.”
Binti huyo alihitimisha kwa kuweka hotuba yake aliyoitoa kwenye kongamano hilo akisema ililenga kuleta umoja na mshikamano.
Tangu
kutolewa kwa kauli hiyo, kumekuwa na mlolongo wa shutuma zinazoelekezwa
kwa binti huyo wa Odinga huku baadhi ya Watanzania wakisaini azimio
maalumu kumtaka ombe radhi ambalo waliosaini wamefikia 17,000.
Tangu
wiki iliyopita, kumekuwapo na mkanda wa video unaosambaa kwenye
mitandao ya kijamii ikimuonyesha Rosemary akihutubia mkutano jijini New
York huku akidai Bonde hilo lililogunduliwa mtu wa kale la Olduvai Gorge
linapatikana nchini Kenya.
Mapema, Serikali ya Tanzania imesema
itachukua hatua za kidiplomasia endapo ungepatikana uhakika juu ya
taarifa zinazoenezwa na mitandao ya kijamii kuwa raia wa Kenya huzitaja
baadhi ya tunu za Tanzania kuwa zinamilikiwa na nchi yao.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambeni alisema hayo alipozungumza
na waandishi wa habari jana akisema Serikali inafanya uchunguzi juu ya
taarifa hizo.
Hata hivyo, alisema hali hiyo inaonyesha ni jinsi
gani nchi Tanzania inazidi kuwa maarufu kwa mazuri yake mpaka majirani
wanatamani miliki zake.
Mwambene alikuwa anazungumzia taarifa za
mitandao zilizowahusisha raia wa Kenya kutamba kuwa Mlima Kilimanjaro,
Olduvai Gorge na Mbuga ya Serengeti vipo nchini Kenya na ripoti za hivi
karibuni kuwa mwanasoka wa kimataifa, Mbwana Samatta na mwanamuziki
Diamond Platinumz ni raia wa Kenya.
0 comments:
Post a Comment