Siku
mbili baada ya baadhi ya wabunge kudaiwa kuhusika katika vitendo vya
rushwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru), Valentino Mlowola amesema taasisi yake inawahoji wote
waliotajwa kuhusika na tuhuma hizo.
Hatua
hiyo imekuja kutokana na tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge wa baadhi ya
kamati za Bunge na kusababisha baadhi yao kuomba kujiuzulu ujumbe
wakishinikiza uchunguzi ufanyike ili waliohusika wawekwe hadharani na
kuchukuliwa hatua.
Mkuu huyo wa zamani wa Intelijensia ya jinai katika Jeshi la Polisi alisema:“Sisi tunachunguza tuhuma zote zinazohusiana na rushwa, kwa maana hiyo tunawachunguza wabunge wote waliotajwa.”
Alisema
uchunguzi huo unakwenda zaidi hadi kuyagusa mashirika ya umma kwa kuwa
lengo ni kushughulikia kashfa ambayo inaweza kuharibu heshima ya Bunge.
Mashirika
ya umma yaliyoguswa katika tuhuma hizo ni Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Alipoulizwa
uchunguzi huo utakamilika lini, alisema hawezi kubashiri kwa kuwa hilo
ni suala la utendaji ambalo linafuata sheria na taratibu.
Wabunge wafunguka
Wakati
Takukuru ikichukua hatua hiyo, wabunge watano waliokumbwa na mabadiliko
ya kuhamishwa kamati yaliyosababisha baadhi yao kupoteza nyadhifa zao
huku yakielezwa kuwa ni ya kawaida, wamefunguka kuhusu uamuzi huo huku
baadhi yao wakiushangaa.
Waliopoteza
nafasi zao kutokana na mabadiliko hayo ni Richard Ndassa, ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Mary
Mwanjelwa (Ardhi, Maliasili na Mazingira), Martha Mlata (Nishati na
Madini).
Waliovuliwa
umakamu mwenyekiti ni Dk Raphael Chegeni (Huduma za Maendeleo ya Jamii)
na Kangi Lugola (Hesabu za Serikali za Mitaa).
Mwanjelwa
alisema inasikitisha na kushangaza kusikia tuhuma zikitolewa kwenye
vyombo vya habari na baadaye kuona mabadiliko ya kamati hizo
yakifanyika.
Alisema kwa sasa bado anatafakari: “Lakini kwa kuwa Spika ndiyo amepewa mamlaka kwa mujibu wa kanuni za Bunge basi huwezi kupinga,” alisema.
Mlata alisema kwa sasa hawezi kuzungumza kauli yoyote kabla ya kuonana na Spika.
Ndasa
alisema Serikali ina mkono mrefu wa kufuatilia na kuchunguza tuhuma
hizo ili kujiridhisha huku akisema mabadiliko yaliyofanyika ni kawaida
na yapo ndani ya mamlaka ya Bunge na hawezi kuhusisha mabadiliko hayo na
tuhuma za rushwa.
Chegeni alikubaliana na mabadiliko hayo huku akibainisha kuwapo kwa kundi la watu wanaojaribu kuchafua taswira ya kamati yake.
“Mabadiliko
ni kawaida tu, anaweza kukupeleka kamati fulani na kukurudisha kamati
yako ya zamani na wala siwezi kuhusisha na tuhuma za rushwa, lakini kama
kuna rushwa kweli lazima iwe na upande wa mpokeaji na mtoaji, mashirika
nayo yachunguzwe na Takukuru kama sehemu ya kuanzia,” alisema.
Zitto Kabwe apongeza
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe amepongeza hatua ya TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja ili kurejesha heshima ya bunge.
0 comments:
Post a Comment