Sunday, March 27, 2016

Ajali ya Lori Yaua watu 7 na Kujeruhi 10

WATU saba wamekufa na wengine 10  k u j e r u h i w a baada ya gari walilokuwa wanasafiri nalo aina ya Mitsubishi Fuso kupasuka tairi la mbele na kugonga kingo za barabara katika barabara kuu ya Igunga-Singida.

Wengi wao walikuwa wafanyabiashara ya samaki waliokuwa wakitokea Igunga kwenda kijiji cha Loya wilayani Uyui, Tabora.

Kutokea kwa ajali na vifo hivyo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Khamis Selemani Issah aliyesema ilitokea majira ya saa tatu usiku katika kijiji cha Nanga, kata ya Nanga wilaya ya Igunga.

Alisema lori hilo lenye namba za usajili T 124 ACS lilibeba abiria wengi kinyume na sheria za usafirishaji wa abiria na kuongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobanika kubeba abiria katika magari ya mizigo.

Mara baada ya ajali hiyo, dereva wake aliyetajwa kuwa ni Joseph Masali alitoweka eneo la tukio na jeshi la polisi linamtafuta aweze kujibu tuhumu zinazomkabili kuhusiana na ajali hiyo.

Kamanda huyo aliendelea kusema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva kutokana na mwendo kasi pamoja na pia kwa kuvunja sheria ya kubeba abiria kwa gari la mizigo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Abdallah Ombeni alipokea majeruhi 11 na miili 6 katika hospital hiyo huku majeruhi mmoja alisafirishwa katika Hospital ya Rufaa ya Nkinga kwa matibabu zaidi kutokana na hali yake kuwa mbaya, hata hivyo alifariki dunia akiwa njiani.

Amewataja waliokufa kuwa ni Masesa Sagalali, Omar Rajabu, Shaaban Ibrahim, Sagalali Maige, Selestine Lipande, Juma Iddi na mwingine aliyetambulika kwa jina mmoja la James. Juma Hassan, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More