Monday, May 21, 2018

Chumi aitaka Serikali kufungua chuo cha Misitu Mafinga

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema ni wakati muafaka sasa umefika kwa Serikali kufungua Tawi la Chuo cha Misitu Olmotonyi katika Mjini Mafinga, Wilayani  Mufindi

NA FREDY MGUNDA

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema ni wakati muafaka sasa umefika kwa Serikali kufungua Tawi la Chuo cha Misitu Olmotonyi katika Mjini Mafinga, Wilayani  Mufindi.

Akichangia katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Chumi alisema kuwa, kwa kuwa madarasa, mabweni na nyumba za waalimu zilishakuwepo, ni muafaka sasa chuo hicho kufunguliwa tena.

Kwa kuwa chuo hicho kilikuwepo na kwa kuwa huku ndiko kuna msitu mkubwa Afrika Mashariki, ni fursa muhimu kwa watu wa Mafinga, Mufindi na Nyanda za Juu Kusini kuwa na chuo cha misitu jambo ambalo pia litarahisisha hata mazoezi kwa vitendo

Aidha mbunge huyo alisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wakala wa Misitu nchini, bado kuna changamoto kadhaa ikiwemo uwepo wa check point nyingi na zuio la malori yanayobeba mazao ya misitu kama mbao kuzuiwa kusafiri usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelekea uchumi wa viwanda, unapokutana na check points zaidi ya kumi kati ya Mafinga na Dar, na unapozuia malori yanayobeba mbao kusafiri usiku, maana yake una slow down speed ya ukuaji wa uchumi, nashauri Serikali iliangalie suala na kama kuna check points basi turuhusu malori yasafiri usiku

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameishauri serikali kuwapa mikataba ya malighafi wavunaji ili waweze kukopesheka.

Kuhusu Utalii, Chumi alisisitiza umuhimu wa Tanapa, Ngorongoro na Bodi ya Utalii Tanzania kupewa fedha za kutosha kwa ajili ya kutangaza vivutio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani asiyeijua coca cola au pepsi, lakini bado wanajitangaza, na sisi iko sababu ya kuongeza nguvu katika kutangaza kwa kuyawezesha mashirika hayo

Akimalizia, Mbunge huyo alisema kuwa kuna sababu ya kubainisha na kutangaza maeneo ya Kihistoria katika Mkoa wa Iringa ambayo walipita au kuishi wapigania uhuru kama vile Nelson Mandela, Sam Nujoma, Thabo Mbeki na wengineo.

Maeneo kama Kihesa Mgagao, tumeweka gereza, badala ya kuifanya historical site ili kuvutia watalii toka kusini mwa Afrika na hivyo kuongeza mapato

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More