Wakati
wanafunzi wa kidato cha pili wakianza mitihani jana, Baraza la Mitihani
la Tanzania (Necta) limetangaza kwamba wanafunzi watakaofeli mtihani
huo hawatorudia darasa, bali wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya
jioni ili kuwawezesha kitaaluma.
Utaratibu
huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles
Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka
wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha
wastani wa alama 30.
Dk
Msonde alisema utaratibu huo mpya utawahusu pia wanafunzi wa darasa la
nne ambao nao hawatalazimika kurudia darasa, bali watakuwa na muda wao
wa ziada wa kusoma.
“Lengo
la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya
ufundishaji. Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na
siyo kuwarudisha darasa tu,” alisema.
Akizungumzia
mtihani huo ulioanza jana, alisema watahiniwa 397,250 walisajiliwa nchi
nzima, wakiwamo wanafunzi 67 wasioona na 224 wenye uoni hafifu.
Mwaka
2008, Serikali ilifuta makali ya mtihani wa kidato cha pili, hali
iliyotoa fursa kwa wanafunzi wengi hata wasio na uwezo kuingia kidato
cha tatu na hatimaye kupata nafasi ya kufanya mtihani wa mwisho wa
kidato cha nne.
Baada
ya matokeo mabaya yaliyotokana na uamuzi huo na pia kelele za wadau wa
elimu na jamii kwa jumla, hatimaye mwaka 2012, Serikali iliurudisha
mtihani huo na kutangaza kuwa wanaofeli watakariri darasa, utaratibu
ambao sasa umefutwa.
0 comments:
Post a Comment