Monday, November 9, 2015

MJUE JAJI DAMIAN ZEFRIN LUBUVA


CHETI chake cha kuzaliwa, kimeandikwa Damian Zefrin Lubuva. Huyu ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambaye alizaliwa Septemba 21, 1940 katika Kijiji cha Haubi Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma.
ELIMU
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Kuta kuanzia mwaka 1949 hadi 1952 na katika Shule ya Kati ya St. Gabriel Catholic Kondoa kuanzia mwaka 1953 hadi 1956.
Baadaye alikwenda Shule ya Sekondari ya St. Francis (Pugu, Dar) mwaka 1957 hadi 1962 ambapo alisoma kidato cha kwanza hadi cha sita. Mwaka 1963 alijiunga na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki (sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ‘Mlimani’) ambapo alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria mwaka 1966.
KAZI
Aprili 5, 1966 aliajiriwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Wakili wa Serikali. Mwaka 1968 alihamishwa kwa muda (seconded) kuwa Mwanasheria wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi hadi 1969. Kati ya mwaka 1969 hadi 1972 alifanya kazi kama Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Arusha na baadaye aliteuliwa kuwa Wakili Mkuu wa Serikali Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Mwaka 1975 hadi 1976 alikuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Sheria Tanzania (Tanzania Legal Corporation).
Mwaka 1976 aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi aliyoendelea nayo hadi mwaka 1977.Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1983. Kati ya mwaka 1984 na 1985 alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Novemba 5, 1985 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania. Mwaka 2008 alistaafu utumishi wa umma. Mwaka 2009 na 2011 alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili la Sekreterieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Desemba 19, 2011 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kazi anayoendelea nayo mpaka sasa.
NYADHIFA NYINGINE
Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Umoja wa Tume za Uchaguzi nchi za Sadc kuanzia mwaka 2012 hadi 2014.
Mjumbe wa Tume ya Mahakama (Judicial Service Commission of Tanzania). Kuanzia 2005 hadi Septemba 21, 2008.
TUMUANGAZIE KWA UNDANI ZAIDI
Mbobezi huyu wa sheria, hakika anastahili tunu ya heshima kwa namna na jinsi ambavyo amelitumikia taifa katika taaluma yake hiyo kupitia vitengo mbalimbali. Umaarufu na weledi wake juu ya masuala ya sheria, umejidhihirisha hivi karibuni katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu uliomalizika siku chache zilizopita.
Jaji Mstaafu Lubuva, amesimamia ipasavyo taaluma yake kwa kufuata vifungu, kanuni na taratibu stahiki na kuhakikisha haki inatendeka pasipo na hujuma ya aina yoyote.
Kati ya vyombo vya utumishi wa kitaifa ambavyo vimepitia misukosuko mingi katika kipindi hiki, ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lakini mzee huyu, ‘alisimamia kucha’ kuhakikisha chombo hicho kinakaa imara pasipo kuyumba.
Msimamo wake haukuwa wa kibinafsi wala ukiukwaji wa sheria, bali alikuwa akiruka viunzi vyote kwa kuweka wazi vifungu vya sheria vinavyofafanua vyema kile anachokisimamia na kukitetea.
MFANO NI HUU
Wakati taifa linajiandaa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu, maneno mbalimbali yaliibuka kutoka kila pembe ya nchi, yakijumuisha wasomi wa sheria, wanasiasa, wanaharakati na wafuatiliaji wa mambo ya haki za binadamu, wakionesha kutokuwa na imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lakini Jaji Lubuva hakutetereka na badala yake alizidi kujiamini na kuwahakikishia Watanzania kuwa, tume ipo imara na imejiandaa vyema kutenda haki na ndivyo ilivyotokea.
Huyu ndiye Jaji Mstaafu, Damian Zefrin Lubuva katika ubora wake.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More