Agizo
la Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu
katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo
zitatakiwa kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Muda
mfupi baada ya kuapishwa na kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya mkuu
wa nchi, Rais alifuta safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali na
viongozi ili kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili hiyo na kuagiza
shughuli hizo zifanywe na mabalozi.
Rais
alisema safari hizo zitadhibitiwa na Ikulu ambayo itatoa kibali kwa
safari maalumu, ikiwa ni pamoja na kuweka masharti ambayo mtumishi
anayetakiwa kusafiri atatakiwa kuyatimiza kabla ya kupewa kibali.
Lakini
utekelezaji wa agizo hilo unakabiliwa na vikwazo vingi, hasa vikubwa
vitano ambavyo ni uchache wa balozi za Tanzania nje ya nchi, ukomo wa
madaraka ya mabalozi, wigo wa ufahamu wa mambo ya kitaalamu na ukosekana
kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili
tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
Idadi ndogo ya balozi
Takwimu
za Umoja wa Mataifa (UN), zinaonyesha kuwa hadi sasa chombo hicho kina
wanachama 193 ambao nchi zinazaweza kuwa na uhusiano nazo wa
kidiplomasia, kwa mujibu wa makubaliano ya wanachama wa umoja huo.
Kwa
mujibu wa wakosoaji, uchache huo utasababisha mabalozi hao kusafiri
sehemu mbalimbali duniani kushiriki kwenye shughuli ambazo viongozi wa
umma walitakiwa kwenda, hali ambayo itasababisha safari kuwapo kama
kawaida isipokuwa wanaosafiri ndiyo watakaobadilika.
“Ni
kweli kwamba idadi ya watu wanaosafiri itapungua, lakini ile dhana ya
safari itabakia vilevile,” alisema mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka
jina lake litajwe.
“Kwa
mfano, mkutano wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Malta, Balozi wa
Tanzania nchini Uingereza ndiye atatakiwa kwenda. Kwa hiyo ni safari
pia.”
Bara
zima la Amerika Kusini lina ofisi moja tu ya ubalozi iliyoko Brasilia,
Brazil, wakati bara la Amerika Kaskazini lina balozi tatu, mbili zikiwa
Marekani--Umoja wa Mataifa jijini New York na Washington--, huku Ulaya
yenye nchi 50 ikiwa na balozi nane, wakati Asia, Arabuni pamoja na
Australia kuna ofisi nane za ubalozi.
Bara la Afrika lenye nchi 52, ndiko kuna balozi nyingi zaidi, kukiwa na ofisi 14.
Ugumu
katika utekelezaji unaosababishwa na idadi ndogo ya mabalozi pia
ulidokezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula mapema mwezi huu.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye alikuwa akijibu
maswali kuhusu vikwazo vitano vya utekelezaji wa agizo hilo la Rais,
alisema suala hilo linaweza kujibiwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Lakini msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga alisema atumiwe ujumbe wa barua pepe ili ajibu suala hilo.
Ukomo wa madaraka ya mabalozi
Suala
jingine linalozungumziwa ni ukomo wa mabalozi katika mamlaka yao, hasa
pale wanapotakiwa kumuwakilishi Rais wakati hawabebi madaraka hayo ya
mkuu wa nchi.
Mara
nyingi wakuu wa nchi huona umuhimu zaidi wa kuwa na mazungumzo baina
yao kuliko na mabalozi inapotokea wamekutana kwenye mikutano ya mikubwa
kama ya Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, Sadc na mingine inayoweka
maazimio muhimu kuhusu masuala kama ya mazingira, afya, na ya
kibiashara.
Lakini Balozi Sefue alisema Rais atakuwa akihudhuria mikutano michache na hivyo uamuzi huo hautaathiri nchi.
“Ni
mikutano michache sana ambayo wanahudhuria wakuu wa nchi,” alisema
Balozi Sefue. “Pale ambapo tutajiridhisha kuwa ubalozi hauwezi
kutuwakilisha vizuri, basi tutaruhusu mtu atoke hapa nyumbani. Hiyo
itakuwa ni baada ya kujua ni nani atakayekwenda na atakwenda kufanya
nini,” alisema Balozi Sefue.
Kwa
uzoefu wake, alisema hata viongozi watakaopewa ruhusa hawatakuwa na
misafara mirefu kama ilivyokuwa awali kwa kuwa wapo baadhi yao ambao
wanakuwa hawafanyi chochote huko waendako.
“Nilipokuwa
Washington niliwahi kushuhudia. Kuna msafara ulikuja, mkubwa sana na
kwa kipindi chote walichokaa pale, wapo baadhi hawakupata nafasi ya
kufanya chochote. Hili nalo ni miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa
katika vibali vitakavyokuwa vinatolewa kwa wale watakaokidhi masharti,”
alisisitiza.
Kuhusu
ukubwa wa ujumbe ambao kiongozi anaruhusiwa kuambatana nao aendapo nje
ya nchi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga amewahi
kufafanua kuwa, kwa mujibu wa itifaki, kila mmoja ana maelekezo yake.
“Msafara
wa Rais hauwezi kulingana na wa makamu wake, Waziri Mkuu au waziri wa
kawaida ambao pia hutofautiana na makatibu wakuu au wakuu wengine wa
idara na vitengo vya Serikali,” alisema Kasiga wakati akitoa ufafanuzi
juu ya gharama za safari za nje wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Uwakilishi wa mamlaka ya Rais
Mbali
na vikwazo hivyo, suala jingine ni mabalozi kubeba majukumu ya Rais
kwenye mikutano ya nje jambo ambalo wakosoaji wanasema litawawia vigumu
hasa watakapotakiwa kufanya uamuzi kwa madaraka ya mkuu wa nchi.
Lakini
Balozi Sefue alisema mabalozi watakaotumwa kwenye mikutano hiyo
watabeba kofia hiyo ya mkuu wa nchi na taarifa itakayotumwa nchini
itakuwa na uzito unaostahili hivyo suala hilo halitaathiri ushiriki wa
nchi.
Mabalozi kutokuwa na utaalamu
Uwezo
wa mabalozi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kitaalamu pia ni
moja ya mambo yanayoonekana kuwa kikwazo kwa agizo la Rais Magufuli
kuzuia safari za nje.
Lakini
Balozi Sefue alisema matukio yanayohusu masuala ya kitaalamu kama
kilimo, mazingira, afya, madini na mawasiliano ambayo yanahitaji
watendaji waliobobea kwenye fani hizo, yatawekewa utaratibu licha ya
kuwa changamoto kwa mabalozi.
“Kila
ubalozi una wataalamu wa masuala mbalimbali ambao wanaweza kutoa
mchango unaostahili kwa lolote linaloweza kuhitajika,” alisema.
“Si
rahisi kukosa mtu mwenye uwezo wa kumsaidia balozi kutekeleza majukumu
yake kiasi cha kuhitaji mtu mwingine kutoka nyumbani. Lakini
likijitokeza hilo, tutatuma mwakilishi.”
Akizungumzia
suala hilo, Balozi Mulamula alisema mapema mwezi huu kuwa utekelezaji
huo utachukua muda kidogo kutokana na balozi nyingi kukosa fedha na
watalaamu.
Suala
la fedha kwenye balozi za Tanzania limekuwa kilio kikubwa kila wakati
wa Bunge la Bajeti na mwaka huu suala hilo liliibuka kwenye hotuba ya
kambi ya upinzani iliyosema kiasi cha Sh30 bilioni ziloizotengwa kwa
wizara hiyo hazikutosha kuwawezesha mabalozi kufanya kazi yao kwa
ufanisi.
Suala
la weledi pia lilizungumzwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ya mwaka
2014/15 ikisema uteuzi holela wa mabalozi usiozingatia sifa,
unalikosesha Taifa fursa nyingi za kiuchumi kwa kuwa wengi hawana
ufahamu wa fursa zilizoko kwenye nchi wanazokwenda.
Lakini
mapema mwezi huu, Balozi Mulamula alisema suala hilo sasa litaangaliwa
kwa jicho la karibu zaidi, hasa uteuzi wa mabalozi.
Alisema
watatoa mwongozo ambao utawataka wawakilishi hao wasibweteke katika
utendaji wao kwa kuwa kuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kupima
matokeo ya utendaji wao kwa kila baada ya kipindi kitakachoelekezwa.
“Kwa sasa tutakuwa tunawapima mabalozi wetu kwa malengo tuliyokubaliana nao ambayo yanaweza kuwa ya mwaka au zaidi.
Tutakuwa tunamuuliza balozi umeweza kuleta watalii au kuwahamasisha wawekezaji wangapi nchini?” alisema.
“Hii ni kwa sababu zamani tulikuwa tunakwenda kienyeji lakini kwa sasa hapa kazi tu.”
Mazungumzo endelevu
Kikwazo
kingine kinachoonekana kwenye utekelezaji wa agizo hilo ni kukosekana
kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili
tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
“Mfano
iwapo kutakuwa na mkutano wa suala fulani la Jumuiya ya Afrika
Mashariki nchini Kenya, kwa agizo hilo la Rais, atakayewakilisha ni
balozi wa Tanzania nchini Kenya,” alisema mkosoaji huyo na kuongeza:
“Iwapo
suala hilo litaendelezwa kwenye mkutano mwingine wa jumuiya nchini
Uganda, ni dhahiri atawakilisha balozi wa Tanzania nchini humo ambaye
hakuwapo kwenye mkutano wa Kenya. Kwa hiyo kutakuwa na upungufu.”
Balozi
Sefue hakutaka kufafanua kuhusu hoja hiyo na badala yake akaielekeza
kwa Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo alisema ina nafasi nzuri zaidi ya
kulizungumzia.
Credit:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment